Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS)
inajenga zaidi ya Kilomita 150 za barabara za magari ya mwendo wa haraka BRT
(Mwendokasi) katika Jijini la Dar-es Salaam.
Hayo yameelezwa katika mkutano wa 16 wa mapitio ya kujadili
masuala ya uchukuzi unaofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha
Arusha (AICC) kuanzia tarehe 5-8 Desemba, 2023.
Akizungumza mbele ya Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa
aliyefungua Mkutano huo, Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu, Mhandisi Ephatar
Mlavi, amesema ujenzi huo wa BRT unatekelezwa kwa awamu sita, ambapo tayari
awamu ya kwanza iliyohusisha barabara za kutoka katikati ya Jiji hadi Kimara
umekamilika na huduma ya usafiri unafanywa na Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka
(UDART), na sasa imeongezwa hadi Mbezi na itafika hadi Kibaha.
Amesema awamu ya pili ni ya barabara ya kutoka katikati ya
Jiji hadi Mbagala, ambayo nayo imekamilika kwa asilimia 99, na sasa wakandarasi
wanamalizia kazi mbalimbali ikiwemo alama za barabarani; na baadaye
itaendelezwa hadi Kongowe; huku awamu ya tatu ikitoka Gongolamboto hadi
katikati ya Jiji, ambayo nayo imeshaanza kujengwa.
Amesema awamu ya nne ni ya barabara ya kutoka katikati ya
Jiji hadi Tegeta, kupitia barabara ya Ally Hassan Mwinyi, na awamu ya tano
itaanzia katikati ya Jiji hadi Tegeta ikihuhusisha barabara ya Nelson Mandela
na Ubungo.
“Awamu ya sita bado inafanyiwa kazi lpo katika hatua ya
upembuzi yakinifu na inapendekezwa kuhusisha barabara za Mwai Kibaki, Morocco
hadi Kawe; Kimara hadi Kibaha; Mbagala hadi Vikindu na barabara nyingine muhimu
za Mkoa wa Dar es Salaam,” amesema Mha. Mlavi.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa barabara hizo zote kutasaidia
kutatua changamoto ya msongamano wa magari katika njia kuu za Jiji la Dar es
Salaam, na kuleta faida kwa magari makubwa yanayosafirisha mizigo kwenye nchi
za Jirani, ambayo kimsingi ndio yenye kuchangia uchumi wa nchi na nchi Jirani
kutembea kwa urahisi na kuleta faida ya kiuchumi.
0 Maoni