Watu wapatao 49 wamekufa na wengine 80 kujeruhiwa wilayani
Hanang’ mkoani Manyara kufuatia kutokea kwa maporomoko ya ardhi katika Mlima
Hanang’ leo asubuhi, yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang’, Janeth Mayanja amesema miili ya
watu hao 49 imehifadhiwa katika hospitali ya Tumaini, na ametoa pole kwa
wananchi wa Hanang’ kwa tukio hilo na kuwataka waendelee kuchukua tahadhari.
Janeth ameeleza kwamba tangu jana zilikuwa zinanyesha mvua za
kawaida wilayani Hanang’ lakini anadhani kwamba mvua hizo zimesababisha kutokea
kwa maporomoko ya ardhi kutoka katika Mlima Hanang’.
“Mvua zimesababisha maporokoko ya ardhi kwenye Mlima Hanang’
ambao pia huwa na chemichemi, maji yaliporomoka kutoka mlima huo yakiwa
yamebeba mawe na miti katika Mji wa Katesh na katika Kata ya Gendabi,” alisema
Janeth.
Amesema hadi sasa maji yanaendelea kutiririka kutoka
Mlima Hanang’ na maji hayo yananguvu yamebeba matope, miti na mawe ukichanganya
na maji ya mvua ambayo mvua inaendelea kunyesha yameleta athari kubwa na
miundombinu imeharibika.
Mkuu wa Wilaya huyo amesema kwamba shughuli za uokoaji
zinaendelea na kuongeza kwamba watu walioathiriwa na maporomoko hayo
watahifadhiwa kwa muda katika shule mbili za sekondari na moja ya msingi.
0 Maoni