Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala
wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) imewasha
Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Ifakara ambacho kimegharimu shilling
bilioni 25.
Akiwasha kituo hicho ambacho kimelenga kuongeza uwekezaji na
uanzishaji wa viwanda kwa upatikanaji wa umeme wa uhakika, Mkuu wa Wilaya ya
Kilombero, Mh Dunstan Kyobya ameshauri kituo hicho kiitwe Samia Ifakara
Substation.
Ameipongeza REA na EU kwa kuhakikisha kituo kimekamilika na
kuwashwa kwani kinaenda kumaliza matatizo ya umeme katika wilaya ya Kilombero,
Malinyi na Ulanga ambayo ni maeneo ya kimkakati ya kilimo na viwanda.
“Tunategemea kuongeza uwekezaji kwa kuanzisha viwanda vya
kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na vile vya kuchakata madini” amesema Mh
Kyobya.
Amewataka wananchi kuhakikisha wanatunza mazingira na vyanzo
vya maji ili kujihakikishia umeme wa uhakika katika mabwawa ya kuzalisha umeme
ya Kihansi na Kidatu.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Jones
Olotu amesema kuwashwa kwa kituo hicho kunaongeza upatikanaji wa umeme na hivyo
kuwawezesha wananchi kukuza na kuboresha hali zao za kiuchumi kwa kufungua
biashara mbalimbali kwa uwepo wa umeme wa uhakika katika maeneo hayo.
“Wananchi watumie upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa
kujiongezea kipato kwa kuwekeza na kuanzisha viwanda vya mazao ya kilimo na
madini ambayo yanapatikana kwa wingi Kilombero, Ifakara, Ulanga na Malinyi,”
amesema Mhandisi Olotu.
Naye Mbunge wa Kilombero, Aboubakar Asenga amewataka
wananchi wa Jimbo hilo kuchangamkia fursa ya upatikanaji wa umeme mkubwa kwa
kuzalisha kwa wingi na kuanzisha viwanda vikubwa.
“Tunaishukuru serikali kwa kutimiza ahadi yake, ni wajibu
wetu wananchi kutumia fursa hii ya upatikanaji wa umeme mkubwa kwa kuwa na
viwanda vya kukausha na kukoboa mpunga, uzalishaji wa matofali kwa kisasa na
uongezaji thamani wa madini ili kujiongezea kipato, ” amesema Mh. Asenga.
Meneja wa Mradi huo kutoka REA, Mhandisi Romanus Lwena
amesema ujenzi wa kituo hicho ulianza 2020 ambapo kinazalisha kV 220 za umeme
baada ya wananchi wa maeneo hayo kuwa wanapata umeme mdogo wa kV 33 uliokuwa
unasababisha kukatika mara kwa mara.
Na baada ya kuwashwa kwa kituo hicho, kutawezesha kuwa na
umeme wa uhakika kwa ajili ya viwanda na shughuli nyingine za kilimo.
Meneja Miradi ya Nishati wa EU, Mhandisi Francis Songela
amesema katika Mradi huo wamechangia shilingi bilioni 18 na Serikali ya
Tanzania imetoa shilingi bilioni 7.
Amesema kituo hicho kipo katika eneo la kimkakati la Mpango
wa Kukuza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania, SAGCOT ambapo Mradi huo unaenda
kuleta mapinduzi ya kilimo na viwanda.
“Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi ni maeneo ya
kimkakati ya SAGCOT kwani yana rutuba kwa kilimo na shughuli nyingi za kiuchumi
ambapo umeme wa uhakika ilikuwa changamoto na kwa kuwashwa kwa kituo hiki
tunategemea mapinduzi ya kilimo na viwanda,” amesema Mhandisi Songela.
Na Mwandishi Wetu, Ifakara-Morogoro
0 Maoni