Naibu Waziri Mkuu na Waziri
wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko ametoa wito kwa wadau wa masuala ya Afya ya
Watoto nchini, kushirikiana kutokomeza tatizo la watoto waliozaliwa kabla ya
wakati (watoto njiti).
Wito huo umetolewa kwa niaba
yake na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe.
Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa hafla ya kusherehekea mafanikio ya Ajenda ya
Mtoto Njiti (2021) iliyofanyika jijini Dodoma.
Amesema takribani watoto
milioni 15 duniani huzaliwa Njiti huku nchi za Bara la Asia na Afrika hasa
kusini mwa jangwa la Sahara, zikiongoza kwa asilimia 80 ya vifo vya watoto hao.
"Inakadiriwa kila mwaka
watoto 336,000 huzaliwa njiti nchini Tanzania na zaidi ya watoto 11,500
hupoteza maisha kutokana na changamoto za kuzaliwa njiti. Ni kweli kwamba
kiwango cha kuzaliwa kwa watoto njiti hapa nchini kimekuwa kikiongezeka. Hatuna
budi kuzidisha mapambano na ningefurahi siku moja itokee taarifa kuwa hakuna
vifo vya watoto njiti nchini kwetu," amesema Waziri Dkt. Gwajima.
Waziri Dkt. Gwajima
ameipongeza Taasisi ya Doris Mollel Foundation kwa kuzindua na kufanikisha
kuhamasisha Wizara ya Afya na wadau wote wanaotoa Bima za afya nchini
kujumuisha gharama za matibabu ya watoto njiti katika mifuko yao ya bima pamoja
na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kujumuisha elimu ya watoto njiti
kwenye masomo ya Sayansi na Baiolojia.
Ameongeza kuwa, Serikali
inaweka mikakati ya namna bora ya kupiga hatua katika masuala ya kiafya kwa
raia na maisha ya watoto nchini lakini ni muhimu kuongeza juhudi za pamoja na
wahisani.
Akizungumza katika hafla
hiyo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Mhe. Ridhwan
Kikwete amebainisha kwamba yeye binafsi akipata nafasi ya kuwasilisha hoja
kuhusu sheria ya utumishi na likizo ya uzazi atashauri likizo ya uzazi ifikie
miezi sita ili watoto njiti wapate malezi stahiki. Ameongeza kwamba sababu za
kuzaliwa watoto njiti ni pamoja na Mila na Desturi pamoja na mimba za utotoni.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Huduma za Ustawi na Maendeleo ya Jamii Mhe. Fatma Toufiq
amesema Taasisi ya Doris Foundation imefanya kazi kubwa na kufikia hatua
Serikal kutenga Bajeti ya kuhudumia watoto hao, hivyo Kamati hiyo itaendelea
kupigania kuhakikisha sheria ya likizo ya uzazi inapita ili mtoto njiti aweze
kupata malezi stahiki. Amewaomba Waheshimiwa Wabunge kupitisha sheria ya
wanawake kukaa miezi 6 baada ya kujifungua watoto njiti na wanaume mwezi mmoja.
Awali Mkurugenzi wa Taasisi
ya Doris Mollel Foundation, Doris Mollel ameelezea lengo la hafla hiyo ni
kujadili namna Serikali na Wadau husika wanavyoweza kufanikisha ajenda kuu ya
kisera ya watoto njiti ambayo ni kurekebishwa kwa sheria ya likizo ya uzazi ya
sasa kutoka siku 84 hadi 180 ambayo ni moja ya ajenda tatu zilizozinduliwa na
Kamati ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii na Doris Mollel Foundation
mwaka 2021.
Na. WMJJWM- Dodoma

0 Maoni