Waziri Mkuu Majaliwa aagiza madeni ya vyombo vya habari yalipwe

 

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kufanya uratibu wa madai yote ya vyombo vya habari serikalini ili madeni yao yaweze kulipwa.

Mhe. Majaliwa ametoa maagizo hayo jana Mkoani Lindi wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Saba wa Mwaka wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, ambapo amesema madeni hayo yaliletwa ofisi yake na kuyafanyia uchambuzi.

“Sisi Ofisi ya Waziri Mkuu iliyachambua madeni yote na wizara zote tuliziandikia barua kali kabisa, na malipo yalianza kulipwa, lakini zipo wizara sugu ikiwamo hiyo aliyoitaja Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri,” alisema Mhe. Kassim Majaliwa.

Kwa hiyo nijukumu lako kuona tasnia ambayo wewe Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari unailea haipaswi kuendelea kulalamika, alisema Mhe. Majaliwa akionesha kuguswa na suala hilo.

Mhe. Majaliwa amemtaka Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari akutane na mawaziri wenzake, makatibu wakuu na wakurugenzi wafanye mapitio madai yote kuona yapi yanalipika ili wanahabari waweze kulipwa madai yao.

“Muweke utaratibu wa kudumu na ambao ni endelevu ili kutatua changamoto hii, kama mmeweka bajeti kwa ajili ya vyombo vya habari na ni jambo muhimu wizara haiwezi kukaa kimya lazima Watanzania wajue, na muache kuwakopa kopo wanahabari,” alisema Mhe. Majaliwa.

Pia, ameiagiza Wizara wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kukamilisha mchakato wa kuandaa kanuni za Sheria ya Huduma za Habari, na maeneo yote yanayohusiana na sheria hiyo hiyo ili ianze kufanyakazi.

Awali, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile alimshukuru Waziri Mkuu wa kuagiza kulipwa madai ya vyombo vya habari, ambapo baadhi yamesha lipwa ila ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) bado hayajalipwa.

Chapisha Maoni

0 Maoni