Wafanyabiashara wanaozalisha
bidhaa na kutoa huduma katika Wilaya ya Nyamagana Jijini Mwanza wamesisitizwa
kuingiza bidhaa wanazozizalosha na huduma wanazozitoa sokoni, baada ya kuzisajili Alama za
Biashara na Huduma hizo kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ili
kujipatia ulinzi wa kisheria na kuhimili ushindani katika soko.
Wito huo umetolewa jana 2023
na Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Hataza kutoka BRELA, Bi. Neema Kitala wakati wa
mafunzo kwa wafanyabaishara wanaozalisha bidhaa na kutoa huduma mbalimbali
kutoka Wilaya ya Nyamagana na kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa Nyakahoja
Jijini Mwanza.
“Uzuri wa kusajili Alama ya
Biashara na Huduma yako ni kukitambulisha kile unachokizalisha sokoni na faida
kubwa utakayoipata ni bidhaa yako kutambulika na kuaminika katika masoko,
bidhaa hiyo kuonekana halali na ya kipekee, pia inakupa faida ya kupenya katika
masoko mbalimbali ndani na nje ya nchi,” amesisitiza Bi. Kitala.
Aidha, Bi. Kitala amefafanua
kuwa, wafanyabiashara wasiposajili Alama za Biashara na Huduma zao, pindi
wanapotambulisha biashara zao sokoni, licha ya kupendwa na watumiaji,
hazitakuwa na ulinzi wa kisheria, hivyo mtu mwingine anaweza akaiga, akasajili
na kuingiza sokoni hivyo kusababisha migogoro ambapo utatuzi wake hutumia muda
na gharama kubwa.
Naye mfanyabiashara wa
chakula cha mifugo Wilayani humo, Bi. Wilhelmina Kubingwa, amesema, mafunzo
hayo yatamuwezesha kusajili Alama ya Biashara anayotumia katika bidhaa zake,
hivyo ili kuweza kushindana katika soko ni muhimu kuweka ulinzi wa bidhaa zake
kwa kusajili Alama anayotumia.
Wakati huohuo, Afisa Sheria
kutoka BRELA, Bw. Calvin Rwambongo, ameongeza kwa kusema kuwa, BRELA inasimamia
Sheria za Miliki Ubunifu ambazo ni Sheria ya Alama za Biashara na Huduma na
Sheria ya Hataza.
Bw. Rwambongo amesema kuwa
Sheria ya Alama ya Biashara inalenga kuwalinda wazalishaji wa bidhaa na huduma
wanaobuni alama, nembo, michoro, ishara mbalimbali kwa lengo la kutofautisha
bidhaa zao wanapoingiza sokoni na Sheria ya Hataza ni haki ya kipekee ya ulinzi
inayompa mbunifu wa bidhaa mpya au mchakato mpya unaolenga kutatua changamoto
za kiufundi.
Ameongeza kuwa, Sheria ya
Alama za Biashara na Huduma iko wazi kwamba Alama inaposajiliwa inazuia wengine
kutumia Alama huaika pasipo idhini ya yule aliyesajili hivyo inamtambua kwa
kumpa ulinzi yule tu aliyesajili na itampa haki yake endapo mtu mwingine
atatumia Alama kama hiyo na kuiingiza sokoni.
Aidha, Rwambongo amewashauri
wazalishaji wa biashara na huduma kukimbilia BRELA kulinda haki zao na
kutotumia Alama za Biashara na Huduma za watu wengine kwakuwa athari yake ni
kubwa ambayo inaweza kusababisha bidhaa zake kuteketezwa na kulipa fidia.
BRELA inatoa mafunzo kwa
Wafanyabiashara kuhusu usajili wa Alama za Biashara na Huduma kuanzia tarehe 13
hadi Novemba hadi 17 Novemba, 2023 katika Wilaya za Nyamagana, Ilemela,
Misungwi na Ukewere Jijini Mwanza.
0 Maoni