Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju amewataka Wakuu wa vyuo vya Elimu ya Juu na Kati kuteua Waratibu Dawati la Jinsia waadilifu, katika kutatua changamoto za ukatili wa kijinsia vyuoni.
Mpanju amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya namna bora
ya uanzishaji wa madawati ya jinsia kwa Wakuu wa Vyuo na Waratibu Madawati ya
Jinsia katika taasisi ya elimu ya juu na elimu ya kati Mkoani Iringa jana.
“Nasisitiza uwezeshwaji wa Madawati hayo ya Jinsia kwa utumia Rasilimali za Serikali au kupitia wadau kuhakikisha madawati haya
yanafikika kiurahisi kwa kuweka mfumo mzuri wa mawasiliano ya utoaji wa taarifa
za ukatili wa kijinsia," amesema Mpanju.
Mpanju ameelekeza wajumbe wa Madawati ya Jinsia kuendesha
Elimu ya kutokomeza matendo ya ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi na wanajamii
ndani ya Vyuo husika kwani kutokomeza matendo ya ukatili na unyanyasaji kwa
wakati kwenye taasisi za Elimu ya juu na ya kati ndio lengo mahsusi la kuundwa
kwa madawati hayo.
"Nitoe rai kwa vyuo vya elimu ya juu na kati
kuhakikisha wanaanzisha ‘Madawati ya Jinsia’ katika vyuo vyao kwa kutumia
Mwongozo wa Uanzishaji, Uendeshaji na Ufuatiliaji wa Dawati la Jinsia wa mwaka
2021 ambao ulishatolewa na unapatikana pia katika tovuti ya Wizara”.
Kwa upande wake, mwezeshaji wa mafunzo hayo Dkt. Cyril Komba
akifafanua mwongozo wa Dawati la Jinsia kwenye Taasisi za Elimu ya Juu na Elimu
ya Kati amesema majukumu yake ya msingi ni kuona ukatili unakomeshwa.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka Ofisi ya
Rais - utumishi Staricko Meshack akitoa mafunzo kuhusu Daftari la Usajili wa
matukio ya ukatili wa kijinsia katika Taasisi za Elimu ya Juu na kati
amesisitiza kutumika kwa madaftari hayo.
Na. WMJJWM- Iringa
0 Maoni