Serikali imeanza kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya
Maendeleo na Huduma kwa Watu wenye Ulemavu ya Mwaka 2004 ili kukidhi mahitaji
yaliyopo.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu, Mhe.Patrobas Katambi ameyasema hayo jana bungeni alipokuwa
akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti maalum (CCM), Mhe. Stella Ikupa
ambaye amehoji mkakati wa serikali kufanya marekebisho ya Sheria namba 9 ya
Mwaka 2010 ya Watu Wenye Ulemavu.
Akijibu swali hilo, Mhe.Katambi amesema mkakati wa serikali
kwa sasa ni kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu
wenye Ulemavu ya Mwaka 2004 ambapo utekelezaji wake umeanza.
Aidha, amesema baada ya kukamilika kwa mapitio ya Sera ya
Mwaka 2004 hatua za marekebisho ya Sheria hiyo zitaanza kwa kuzingatia
mapungufu yatakayobainishwa katika tathmini ya utekelezaji wa Sera hiyo.
Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Viti maalum (CCM),
Mhe.Mariam Kisangi amehoji serikali imejipangaje kutoa elimu kwa watu wenye
ulemavu ili kutoa maoni kwenye mapitio hayo.
Mhe.Katambi akijibu swali hilo, amesema mapitio ya sera
yanatarajiwa kukamilika Mwaka huu na yamekuwa shirikishi kwa makundi yote ya
watu wenye ulemavu.
0 Maoni