Mwanamke apandishwa kizimbani Mwanza kwa kosa kutumia bangi

 

Mkazi wa Lumala wilayani Ilemela mkoani Mwanza, Salma Abdallah (37), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya hiyo na kusomewa shtaka la kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya aina ya bangi.

Salma amesomewa shtaka hilo katika kesi ya Jinai namba 152/2023 ambapo anadaiwa kutenda kosa hilo kinyume na Kifungu namba 17 (1) (b) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Sura ya 95 toleo la Mwaka 2019.

Akimsomea shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Amani Sumari, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Monika Mweli amesema mshtakiwa alitenda kosa hilo kati ya tarehe 1.10.2023 na tarehe 27.10.2023, eneo la Lumala Wilaya ya Ilemela.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, mshatakiwa amekana na kurejeshwa rumande kutokana na kutokidhi masharti ya dhamana ambapo alitakiwa kuwa na wadhamini wawili na kila mmoja kusaini bondi ya maneno ya shilingi milioni mbili kwa kila mmoja, kitambulisho pamoja na barua ya mwenyekiti wa serikali ya mtaa ambapo mshtakiwa alijibu hana wadhamini hao.

Hakimu, Sumari ameahirisha shauri hilo hadi tarehe 13.11.2023 litakapokuja kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali ya shtaka linalomkabili.

Chapisha Maoni

0 Maoni