Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani Dkt.Frank-Walter Steinmeier amewaomba radhi Watanzania kuhusu ukatili wa wajerumani wakati wa Vita vya MajiMaji na kuahidi kutafuta majibu ya maswali magumu kuhusu vita hivyo ili kujenga mahusiano mazuri zaidi baina ya Tanzania na Ujerumani.
Rais Dkt.Steinmeier ametoa kauli hiyo leo tarehe 1 Novemba
2023 wakati alipotembelea Makumbusho ya Vita vya Majimaji ambapo amejifunza
historia ya vita hivyo na kupata fursa ya kutembelea na kuweka shahada ya maua
kwenye kaburi la halaiki la Mashujaa 66 walionyongwa na Wajerumani na kaburi la
kiongozi wa vita hivyo Nduna Songea Mbano.
"Vile vile, ana kwa ana, ninaomba msamaha kwa mambo
yote ambayo Wajerumani waliwatendea mabibi na mababu zenu hapa," amesema
Mhe. Rais
Amesisitiza kuwa amefurahi kujifunza historia ya Shujaa
Songea Mbano kwa undani na kukutana na familia ambapo amesema kinachomgusa ni
namna ambavyo Watanzania wanahuzunika kuhusu historia ya Mashujaa na namna
ilivyoathiri vizazi vilivyopo.
Ameongeza kuwa ni Wajerumani wachache wanaoifahamu historia
ya vita vya MajiMaji hivyo amefika katika Makumbusho ili akawaeleze Wajerumani
historia ya matukio yaliyotokea huko nyuma kwa lengo la kuendelea kujenga na
kuboresha historia njema siku za usoni baina ya Tanzania na Ujerumani.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas
Ndumbaro ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Songea Mjini ameomba Serikali ya
Ujerumani kujenga jengo kubwa la Makumbusho ya kisasa kuhusu historia ya Vita
vya MajiMaji.
Aidha, ameomba ushirikiano baina ya mji wa Songea na mji
mwingine wa Ujerumani kwa lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano.
"Tunaamini ushirikiano wa kiuchumi na kijamii ndio
utakuwa daraja zuri la kujenga mahusiano mazuri na kuondoa historia mbaya ya
siku za nyuma," amesema Mhe Dkt. Ndumbaro.
Naye Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan
Kitandula amesema Wizara yake inathamini mchango unaotolewa na Taifa la
Ujerumani hususan kwenye eneo la mafunzo na utafiti mbalimbali kwenye masuala
ya Malikale.
Mhe. Kitandula amesema kuwa Serikali ya Tanzania ipo tayari
kwa majadiliano ya namna ya kutumia Vita vya MajiMaji kwa faida ya mataifa yote
mawili.
0 Maoni