SERIKALI kupitia Mamlaka ya
Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) katika kipindi cha mwaka 2022/23
imetoa zaidi ya Billioni Mbili kwa Halmashauri ya wilaya ya Babati na Jumuhiya
ya Uhifadhi ya Wanyamapori Burunge (JUHIBU) ikiwa ni kurejesha kwa jamii faida
zitokanazo na shughuli za utalii zinazofanywa na TAWA wilayani humo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa
Wilaya ya Babati Mhe. Lazaro Twange wakati wa ziara ya kutembelea miradi ya
maendeleo itokanayo na gawio linalopatikana kutokana na shughuli za uwindaji wa
kitalii na utalii wa picha iliyofanywa na TAWA Mkoani Manyara
"Pato linalopatikana
kutokana na shughuli za uhifadhi pamoja na makato mengine yanayosambaa maeneo
mengi, kiwango kikubwa sana kinarudi kwa wananchi" amesema Mhe. Twange.
"Kwa mfano siku za hivi
karibuni hii Jumuhiya ya hifadhi ya Wanyamapori Burunge iliyopo hapa kwangu
Babati wamepata zaidi ya Shillingi Bilioni mbili ambazo zimegawanywa katika
vijiji vyote kumi" ameongeza.
Mhe. Lazaro amesema kutokana
na fedha hizo zipo Zahanati zimejengwa mpaka zimetimia na kuwekewa vifaa tiba
pia miradi mingine kama nyumba za waganga, mabweni katika shule ya Sekondari
Mbugwe na miradi mingine mingi
Aidha, Mkuu huyo wa wilaya
ameipongeza TAWA kwa kazi kubwa inayofanya wilayani humo kiasi cha kupelekea
ujangili kupungua kwasababu wananchi wanaona manufaa ya moja kwa moja
yanayotokana na shughuli za uhifadhi na utalii
Naye Mkurugenzi wa H/W ya
Babati Anna Mbogo amesema kupitia mapato ya utalii wa picha na uwindaji wa
kitalii asilimia kumi ya mapato hayo huwa inarudi katika ngazi ya Halmashauri
na asilimia 65 inapelekwa katika Jumuhiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge
ambayo ina jumla ya vijiji kumi na asilimia 25 kubaki TAWA, ambapo fedha hizo
hutumika katika miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya jamii.
Akifafanua mgawanyo wa fedha
hizo, Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja amesema katika kipindi cha Mwaka
2022/23 Halmashauri ya wilaya ya Babati ilipata zaidi ya Millioni Mia tatu na
Jumuhiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge zaidi ya Bilioni Mbili fedha ambazo
zimetokana na shughuli za utalii.
Aidha, amewaomba wananchi
kushirikiana na Mamlaka hiyo katika ulinzi wa rasilimali za Wanyamapori ikiwemo
kulinda na kutunza mazingira kwani pasipo uhifadhi imara shughuli za utalii
zitazorota na hivyo kulikosesha Taifa pato ambalo lingeweza kuongeza miradi
mingi ya maendeleo katika jamii mbalimbali nchini.
Na Beatus Maganja
0 Maoni