SERIKALI imezitaka Jumuiya
za Kimataifa zisaidie kukuza uchumi wa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania ili
kupanua wigo wa ushiriki wa wananchi wake.
“Tumeliomba jukwaa hili
lione namna ya kushirikisha nchi zinazoendelea kuboresha uchumi wetu ndani ya
nchi kwa kukuza biashara na milango ya uwekezaji na namna nyingine zinazoweza
kusaidia kuinua uchumi wetu,” amesema.
Hayo yamesema leo (Ijumaa,
Novemba 17, 2023) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akiwasilisha tamko la
Serikali kwenye ufunguzi wa mkutano wa pili wa Jukwaa la Sauti za Nchi
Zinazoendelea uliofanyika kwa njia ya mtandao chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu
wa India, Narendra Modi.
Akizungumza kwa niaba ya
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Majaliwa ameliomba jukwaa hilo
liangalie namna linavyoweza kushirikisha uchumi wa dunia na kuufungamanisha na
uchumi wa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.
Akielezea kuhusu masuala
mengine, Waziri Mkuu ameliomba jukwaa hilo lihakikishe linatafuta majibu ya
changamoto za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, masuala ya nishati
mbadala, uwezeshaji wa vijana na wanawake
Jukwaa hilo linaziwezesha
nchi zinazoendelea kujadili changamoto zinazowakabili na kupaza sauti zao ili
ziweze kuwasilishwa kwenye mkutano wa kundi la nchi 20 zenye maendeleo makubwa
ya kiuchumi (G20) utakaofanyika Novemba 20, mwaka huu.
Mapema, akifungua mkutano
huo, Waziri Mkuu wa India, Bw. Modi alisema licha ya kwamba jukwaa hilo lina
wanachama zaidi ya 100, bado wote wanaunganishwa na mahitaji na vipaumbele
ambavyo vinafanana.
“Desemba, mwaka jana, India
ilichukua uenyekiti wa G20 lakini tukajipa jukumu la kuhakikisha sauti za nchi
zinazoendelea zinasikika na ndiyo maana tukaandaa mkutano wa kwanza wa Jukwaa
la Sauti za Nchi Zinazoendelea (Voice of Global South Summit -VOGSS) ili tuweze
kupaza sauti zetu kwa mataifa tajiri na mfano ni kuzindua umoja wa watumiaji wa
nishati mbadala (Global Biofuel Alliance).”
Mkutano wa leo umeshirikisha
wakuu wa nchi na wawakilishi 13 wakiwemo marais sita ambao ni Rais Sitiveni
Ligamamada Rabuka (Fiji), Rais Joko Widodo (Indonesia), Rais Dkt. William Ruto
(Kenya), Rais Sadyr Nurgojoevich Japarov (Jamhuri ya Kyrgyz), Rais Richard
Ravalomanana (Madagascar) na Rais Daviv Adeang (Nauru).
Mawaziri Wakuu walioshiriki
mkutano huo ni Bibi Sheikh Hasina wa Bangladesh, Dkt. Abiy Ahmed Ali
(Ethiopia), Bw. Pravind K. Jugnauth (Mauritius), Bw. James Marape (Papua New
Guinea), Bw. Ferdinand Marcos (Philippines) na Mshauri Mkuu wa Serikali ya
Mpito ya Bhutan, Bw. Chogyal Dago Rigdzin.
0 Maoni