Jeshi la Polisi nchini
limezitaka kampuni binafsi za ulinzi zisizo na sifa ya kutoa huduma ya ulinzi
kusitisha mara moja hadi zitakapokidhi vigezo.
Marufuku hiyo imetolewa na
Mkuu wa usimamizi wa kampuni binafsi za ulinzi kutoka makao makuu ya jeshi la
polisi Kamishna msaidizi mwandamizi wa polisi (SACP) Urich Matei akiwa jijini
Mwanza kwenye kikao kazi kilicholikutanisha jeshi hilo na wamiliki na wasimamizi
wa kampuni binafsi za ulinzi.
SACP Matei amempongeza Kamanda
wa Polisi mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa kwa hatua ya kufanya vikao vya
mara kwa mara na wamiliki wa makampuni hayo na kuweka mikakati ya kuhakikisha
wanafanya shughuli zao kwa ufanisi.
"Natoa pongezi za dhati
kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi
(SACP) Wilbrod Mutafungwa kwa kikao alichokifanya wiki mbili zilizopita
nilikiona kupitia vyombo vya habari kati ya Jeshi la Polisi na kampuni binafsi
za ulinzi kilikuwa kizuri sana," amesema SACP Matei.
Ameongeza "Aliweka
mikakati ambayo wote tumezingatia ili kukabili changamoto zinazotukuta,
hongereni sana.”
Katika hatua nyingine SACP
Matei ametoa rai kwa Makamanda wa Polisi nchini kuiga mfano wa Kamanda
Mutafungwa na timu yake kwa kufanya vikao na kampuni binafsi za ulinzi.
"Nitoe rai kwa
makamanda wote wa Jeshi la Polisi nchini, kupitia kitengo cha Polisi Jamii
watoke ofisini na wasaidizi wao kwenda kwenye maeneo yao ili kupata takwimu
sahihi ya kampuni zinazofanya kazi kwenye maeneo yetu na askari wanaolinda
pamoja na kumbukumbu zao" amesema Matei.
Kwa upande wake, Afisa
Polisi Jamii Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Ramadhani
Sarige ameahidi kuendeleza usimamizi thabiti kwa kampuni hizo ikiwa ni pamoja
na kuchukua hatua za kisheria kwa kampuni zitakazo shindwa kufuata sheria
Amani Nasoro ni Mkurugenzi
wa Kampuni binafsi ya ulinzi ya Amaka ameliomba Jeshi la Polisi nchini
kuanzisha kitengo cha kutoa elimu kwa walinzi wa kampuni binafsi za ulinzi ili
kuwa na watendaji wanaofanana kama askari Polisi walivyo Mikoa yote.
"Askari wa Mkoa wa Katavi na wa Mwanza
wako sawa kiutendaji lakini askari wa kampuni binafsi za ulinzi hawafanani
kiutendaji kutokana na tofauti ya
mafunzo wanayoyapata sehemu tofauti," amesema Amani.
0 Maoni