Wakala wa Usajili wa
Biashara na Leseni (BRELA), imepongezwa kwa hatua ya kuwanoa wafanyabiashara wa
Mwanza kwa kuwapatia elimu ya Usajili wa Alama za Biashara na Huduma kwa kuwa
wengi huzalisha na/au kuingiza bidhaa sokoni bila kufahamu umuhimu wa sajili hizo.
Pongezi hizo zimetolewa jana
na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana, akimwakilisha Mkuu wa
Mkoa huo Mhe. Amos Makalla, wakati Maafisa wa BRELA walipokwenda Ofisini kwakwe
kujitambulisha.
Kaimu Mkuu wa Sehemu ya
Hataza Bi Neema Kitala, akimwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, ameeleza
kuwa Taasisi imedhamiria kuwajengea uwezo wazalishaji na wafanyabiashara wa
bidhaa na huduma mbalimbali kwa lengo la kuwawezesha kulinda Alama zao na
kuhimili ushindani katika masoko ya ndani na nje, kuaminika na walaji na zaidi
kuwaepusha kuingia kwenye migogoro.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti washiriki wa Mafunzo hayo kutoka Wilaya ya Ilemela wameelezea
kuridhishwa na huduma za BRELA.
Meneja wa Kampuni ya
Joasamwe inayozalisha gundi ya karatasi, Bi. Fauzia Ibrahim amesema kuwa
walianza uzalishaji baada ya kusajili Kampuni yao, hata hivyo walikumbana na
changamoto ya kutumia nguvu kubwa ya kutambulisha bidhaa yao sokoni.
“Bidhaa ya gundi ya karatasi
inazalishwa ndani na nje ya nchi na bidhaa hiyo ni nyingi sokoni, kutokana na
elimu tuliyopata tutachukua hatua ya haraka kusajili Alama yetu ya biashara ili
iweze kujulikana na kutofautishwa na washindani wetu kwakuwa bidhaa yetu ni
bora zaidi,” amesema Bi. Ibrahim.
Kwa upande wake Bw. Salum Ramadhani ameeleza kuwa
changamoto kubwa waliyonayo ni kutokuwa na ufahamu wa usajili wa Alama za
Biashara, kwani walijua usajili ni wa Kampuni pekee, lakini kupitia Mafunzo
hayo wamepata uelewa na watasajili Alama za Biashara ambazo zitakuwa na upekee
na zenye kutambulisha bidhaa zao.
Naye Bi. Salome Nyakwaka
ameishukuru BRELA kwa kutoa elimu ya Alama za Biashara na Huduma kwakuwa wengi
walikuwa hawajui umuhimu wa kusajili Alama zao na wengi wanazalisha bidhaa kwa
kuweka Alama zenye mfanano bila kufahamu athari ya kutumia Alama hizo.
BRELA inasimamia Sheria za
Miliki Ubunifu ambazo ni Sheria ya Alama za Biashara na Huduma pamoja na Sheria
ya Hataza. Sheria ya Alama za Biashara na Huduma inalenga kuwalinda wazalishaji
wa bidhaa na huduma wanaobuni alama, nembo, michoro, ishara mbalimbali kwa
lengo la kutofautisha bidhaa au huduma zao wanapoingiza sokoni, na Sheria ya
Hataza inatoa haki ya kipekee ya ulinzi inayompa mbunifu wa bidhaa mpya au
mchakato unaolenga kutatua changamoto za katika jamii.
0 Maoni