Licha ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini (HESLB), kuwawezesha
mikopo wanafunzi zaidi ya 750,000 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2004, bado
inakabiliwa na tatizo la urejeshaji mikopo kwa hiyari.
Mkurugenzi Mkuu wa bodi hiyo, Bw. Abdul-Razaq Badru ameyasema
hayo leo jijini Dar es Salaam katika mkutano wake na Wahariri wa Vyombo vya Habari, chini
ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
“Bodi ya mikopo ipo katika hatua ya
kuunganisha mfumo wake na taasisi zingine za Serikali ikiwemo wa Hifadhi za
Jamii na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ili kuhakikisha inawapata wale wote
waliokopa kwenye bodi hiyo,” amesema Bw. Badru
Kuhusu makusanyo ya mikopo, Bw. Badru amesema hadi kufikia Septemba
2023, fedha zilizokusanywa na HESLB kutoka kwa wakopaji zaidi ya 230,000
zinakadiriwa kufika Tsh. 1.3 trilioni.
Akizungumzia wanufaika wa mikopo Bw. Badru amesema katika
mwaka 2023/24 kuna jumla ya wanufaika 229,652 wa mikopo wanaochukua shahada, Samia
Scholarship na Diploma, waliotengewa kiasi cha shilingi bilioni 786.
0 Maoni