Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Itikadi na
Ueneza Bw. Paul Makonda, amewatumia salamu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa pamoja na Watendaji
wote wa Serikali kuwa chama hakitosita kuwachukulia hatua iwapo watabainika hawajafanya
kazi yao kikamilifu.
Bw. Makonda ametoa kauli hiyo leo Jijini Dar es Salaam, wakati
walipopokelewa katika Ofisi za Ndogo za CCM Lumumba, baada ya kuteuliwa katika
nafasi hiyo tarehe 22/11/2023 pamoja Rabia Abdallah Hamid Katibu wa Halmashauri
Kuu ya CCM Taifa, Siasa na Mahusiano ya Kimataifa.
“Ninatuma salamu kwa Mawaziri na Wakuu wa Mikoa wote, kuwa
kila mtu ataubeba msalaba wake na kwa bahati nzuri tunajuana,” alisema Makonda
na kuongeza “Sitakuwa msemaji wa chama muongo, sijafunzwa kwa miaka mitatu na miezi
mitatu ili nije kusema uongo.”
Akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya kupotea kwenye
medani za kisiasa kwa muda wa miaka mitatu na miezi mitatu, Bw. Makonda amesema
kiongozi yeyote atakayebainika kuzembea katika kutekeleza majukumu yake CCM
itamchukulia hatua.
Kuhusu suala la baadhi ya watu kudhani kuwa baada ya
kuteuliwa kwenye nafasi hiyo kuwa atalipa kisasi, Makonda amewatoa hofu kwa
kusema “Mimi sina kisasi na mtu yeyote na asiwepo mtu akafikiri lengo langu
litakuwa ni kumkandamiza.”
Akiongelea kuhusu watu waliokuwa wanawaza kuwa Makonda
atakuja na mambo gani, amesema kwamba yeye hana ya kwake, anayo ya CCM ambayo
yanaongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Samia Suluhu Hassan.
“Ninajua kuwa Watanzania wanatufuatilia katika vyombo vya
habari, na wengi wanataka kujua leo Makonda atasema nini na wengine wameenda
mbali zaidi na kusema tuone dira, maono na shabaha yake,” alisema Makonda na
kuongeza, “Nataka niwaeleze kuwa hakuna maono ya Makonda, kuna maono na malengo
ya CCM, tuna Ilani yenye zaidi ya kurasa 300 jukumu letu ni kuitekeleza na
kuielezea.”
Kuhusu upinzani Bw. Makonda amedai kuwa Tanzania haina chama
cha upinzani ila inawatoa taarifa waliojikusanya katika vyama vya watoa taarifa,
“Tanzania haina chama cha upinzani, Tanzania inawatoa taarifa. Ukimuona Tundu
Lissu anaongea sio chama ni mtu tu anatoa taarifa”.
Kuhusu mikutano ya hadhara, Makonda amesema amemuona Mwenyekiti
wa Chadema Taifa Freema Mbowe akihutubia mikutano kwa kutumia Helkopta, hii inatokana
na dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza Demokrasia na Uhuru wa watu
kujieleza.
Aidha, Bw. Makonda amesema kwa utumia mamlaka aliyonayo
anawaagiza wanaohusika na mamlaka ya vibali wampee Mbowe kibali cha kuruka na helkopta
na kama ameishiwa na mafuta aseme tu kwa kuwa tayari ameshamuombea kwa Mhe. Rais
Samia na amekubali kumchangia mafuta.
0 Maoni