TIB yawekeza 980.7bn na kuzalisha ajira zaidi ya 30,000

 

Banki ya Maendeleo TIB, imefanya uwekezaji wa kiasi cha fedha shilingi bilioni 980.7 kwenye miradi ya sekta ya binafsi na sekta ya umma nchini hadi kufikia Septemba 30, 2023 na kuzalisha ajira zaidi ya 30,000.

Mgawanyo wa uwekezaji huo ni kama ifuatavyo asilimia 93% ya miradi ni ya sekta binafsi, asilimia 7% ya miradi ni ya sekta ya umma, ambapo asilimia 80% ya miradi hiyo ni miradi ya muda mrefu zaidi ya miaka 5.

Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TIB Lilian Mbassy leo Dar es Salaam wakati akiongea na Wahariri wa vyombo vya habari, katika mwendelezo wa mikutano ya taasisi za umma inayoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

“Jumla ya miradi 253 ya sekta kilimo ya usindikaji wa mazao ya kilimo imekopeshwa kwa kutumia kiasi cha shilingi bilioni 334.7 kilichowekezwa,” amesema Mbassy na kuongeza, “Mikoa 23 na wilaya 76 imenufaika na uwekezaji huo ambao umezalisha ajira 10,230 kwa wananchi.”

Amesema jumla ya miradi ya maji 66 imekopeshwa, ikihusha Mamlaka za maji 6 na Jumuiya za Watumia Maji Vijijini 60, ambayo imepatiwa kiasi cha shilingi 14.9 na kuwanufaisha wananchi 750,000.

Kwa upande wa sekta ya nishati Bi. Mbassy amesema kiasi cha shilingi bilioni 12.03 kimewekezwa kwenye miradi sita katika mikoa mitano nchini na kuzalisha jumla ya Megawati 8.84 kwa kaya 500,000.

Ametaja mikopo iliyotolewa na TIB kisekta kuwa Kilimo/Usindikaji shilingi 334,686,590,203.02, Madini na Uchakataji shilingi 205,393,327,423.00., Utalii shilingi 154,959,105,050.00, Viwanda shilingi 119,297,697,881.00 na Huduma nyingine shilingi 70,049,373,967.62.

Pia, Ujenzi na Majengo shilingi 45,338,526,515.00, Maji na Afya shilingi 14,898,020,726.00, Elimu shilingi 14,823,606,477.00, Umeme na Nishati shilingi 12,037,600,747.00, Usafiri na Mawasiliano shilingi 5,488,118,156.00 na Washirika wa Kifedha 3,721,238,913.00.

Benki ya Maendeleo TIB (iliyokuwa inajulikana kama Tanzania Investment Bank) ilianzishwa kama Taasisi ya Fedha ya Maendeleo (Development Finance Institution - DFI) kwa mujibu wa Sheria namba 20 ya mwaka 1970 iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Tarehe 6 Novemba, 1970.

Chapisha Maoni

0 Maoni