Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu
Hassan, ameshuhudia utiaji saini wa mikataba mahususi mitatu ya uwekezaji na
uendelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam katika hafla iliyofanyika katika Ikulu
ya Chamwino Jijini Dodoma.
Mikataba hiyo ya uwekezaji baina ya Mamlaka ya Bandari
Tanzania (TPA) na Kampuni ya DP World ya Dubai ni pamoja na Mkataba baina ya
Serikali, Mkataba Uendeshaji Gati namba 4 hadi namba 7 pamoja na Mkataba wa
Upangishaji Gati namba 4 hadi namba 7.
Akiongea katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Rais wa
Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi, Rais Samia amesema katika makubaliano hayo maslahi
mapana ya nchi yamezingatiwa na kuwahakikishia Watanzania kwamba maoni yao yote
mazuri waliyoyatoa yamezingatiwa kwenye mikataba hiyo.
“Serikali ilisikiliza michango na maoni mbalimbali
iliyotolewa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Vyama vya Siasa, Asasi za
Kiraia, Wanaharakati Huru, Vyombo vya Habari na pia tumeangalia pia maoni
yaliyotolewa kwenye mitandao ya jamii,” amesema Rais Samia na kuongeza
“Tumewasikiliza pia Viongozi wetu wa dini
na baadhi ya Viongozi wetu wastaafu, tumefuatilia kwa karibu sana hoja
za Waheshimiwa wabunge wakati wa kujadili na kupitisha azimio la bunge na
tulipokea pia ushauri wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM.”
Amesema Bandari ya Dar es Salaam ni moja ya kiunganishi
muhimu cha kibiashara kati ya Tanzania na mataifa mengine, kwa kuwa inahudumia
shehena kubwa ya mizigo ya nchi jirani na hata mataifa ya mbali, hivyo
maboresho yakiutendaji yatayofanywa kwa uwekezaji huu yatakuza biashara za
ndani na nje na kuchangia katika uchumi wa taifa.
Awali wakati akimkaribisha Rais Samia, Makamu wa Rais Dkt.
Philip Mpango alisema kuwa uwekezaji huo ni muhimu kutokana na ukweli kwamba
Bandari ya Dar es Salaam inakabiliwa na ushindani wa bandari ya Mombasa Kenya,
Msumbiji, Afrika Kusini pamoja na nyingine Afrika ya Magharibi.
“Bandari yetu ispokuwa na tija biashara inakwenda huko
kwingine, kwa hiyo ni lazima tujidhatiti tupambane kiushindani, na tukio hili
la leo Mheshimiwa Rais wewe ni jasiri kweli kweli, tukio la leo ni kuipeleka
nchi yetu ili tukashindane kibiashara kwenye bandari.” alisema Dk. Mpango.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari
Tanzania (TPA) Plasduce Mbossa alisema kuwa mkataba wa DP World wa uendelezaji
na uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam ni wa miaka 30 na utendaji kazi wa DP
World utakuwa ukipimwa kila baada ya miaka mitano.
0 Maoni