Madaktari Bingwa wa JKCI wapatiwa mafunzo India

 

Wataalamu wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wako nchini India kwaajili ya kujifunza upasuaji wa kubadilisha valvu ya mshipa mkubwa wa damu (Aortic Valve) pasipo kufanya upasuaji wa kufungua kifua (Transcatheter Aortic Valve Implantation procedure – TAVI).

Upasuaji huo unafanyika kwa njia ya tundu dogo kupitia mtambo wa Cathlab ambao ni maabara inayotumia mionzi maalumu kwaajili ya kufanya uchunguzi na matibabu ya moyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu leo jijini Dar es Salaam daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI ambaye yuko nchini India katika mafunzo hayo Khuzeima Khanbhai alisema upasuaji wa aina hii haufanyiki hapa nchini lakini kutokana na teknolojia ya matibabu kukuwa Taasisi hiyo imeona iwapeleke wataalamu wake kujifunza nchini India.

“Tuko wataalamu wanne ambao kwa muda wa wiki moja tutakuwa hapa India kujifunza aina hii ya upasuaji, wawili ni madaktari, muuguzi mmoja na mtaalamu wa kuendesha mtambo wa Cathlab mmoja,” alisema Dkt. Khuzeima.

“Upasuaji huu haufanyika hapa nchini kwani ni teknolojia mpya na ya kisasa ya matibabu ya moyo ambayo inatumika katika nchi zilizoendelea lakini kwakuwa katika Taasisi yetu tunavifaa vya kisasa Serikali imeona ni muhimu na sisi tukajifunza ili tuweze kutoa huduma hii kwa watanzania wenye matatizo ya moyo,” alisema Dkt. Khuzeima.

Dkt. Khuzeima alisema upasuaji wa TAVI unafanyika kwa wagonjwa wenye matatizo ya Valvu za moyo wenye umri wa kuanzia miaka 70 na kuendelea au kwa watu ambao ni wagonjwa sana na hawawezi kustahimili upasuaji mkubwa wa kufungua kifua.

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inafanya upasuaji wa kubadilisha valvu ya mshipa mkubwa wa damu (Aortic Valve) kwa njia ya upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua. Kuanza kufanyika kwa upasuaji mdogo wa TAVI kutawasaidia wagonjwa wenye umri mkubwa au wagonjwa sana na hawawezi kustahimili upasuaji mkubwa wa kufungua kifua kufanyiwa upasuaji huo hapa nchini na hivyo Serikali kupunguza gharama za kuwapeleka wagonjwa hawa kutibiwa nje ya nchi.

Chapisha Maoni

0 Maoni