Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeonyesha
utayari wa kuendelea kuimarisha masuala ya uwekezaji, mafunzo na matumizi ya
teknolojia katika kukuza sekta ya utalii kwa kufanyia kazi miongozo inayotolewa
na Shirika la Utalii Duniani (UNWTO).
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Jasmine Kairuki
(Mb), amesema hayo baada ya kushiriki Jukwaa la Uwekezaji (Global Investment
Forum) lililofanyika sambamba na Mkutano Mkuu wa 25 wa Shirika la Utalii
Duniani (UNWTO) unaoendelea jijini Samarkand, Uzbekistan.
Katika mijadala iliyowasilishwa, nchi wanachama
zimesisitizwa kuzingatia uwekezaji endelevu unaozingatia utunzaji wa mazingira,
kuimarisha uwekezaji katika eneo la mafunzo na matumizi ya teknolojia ili
kuendelea kuboresha sekta ya utalii na ukarimu.
Aidha, nchi wanachama zimesisitizwa kuendelea kuboresha
miundombinu ili kuvutia watalii wengi zaidi.
Waziri Kairuki pia alitembelea maonesho ya utalii yaliyokuwa
yakifanyika sambamba na Jukwaa la Uwekezaji na kujionea vivutio na maendeleo ya
utalii nchini Uzbekistan na kushauri wadau wa utalii nchini Uzbekistan
kutangaza utalii na bidhaa zao nchini Tanzania ikiwemo kuchangamkia fursa ya
maonesho ya kimataifa yanayofanyika nchini Tanzania.
Katika hatua nyingine, Mhe. Waziri alikutana na kufanya mazungumzo
na Bw. Raximov Jurabek Raximovich, Gavana wa Jimbo la Khorezm, ambalo limepiga
hatua kubwa katika utalii wa utamaduni na ubunifu katika kazi za sanaa za
mikono (handcrafts).
Kupitia mazungumzo
hayo, Mhe. Kairuki alitoa pendekezo kwa nchi mbili kushirikiana katika kukuza
utalii ikiwemo kubadilishana uzoefu katika kukuza utalii wa utamaduni,
kuimarisha usafiri wa anga kati ya nchi mbili ili kurahisisha watalii
kutembelea nchi zote mbili pamoja na kuimarisha ushirikiano wa wadau wa utalii
kutoka sekta binafsi kwa lengo la kukuza utalii katika nchi zote mbili.
0 Maoni