Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii
imeishauri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kupitia
Kitengo cha Huduma za Ajira kupanua wigo wa fursa za ajira kwa Watanzania nje
ya nchi.
Akizungumza jana katika kikao cha kamati hiyo cha kupokea na
kujadili utendaji kazi wa kitengo hicho, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Fatuma
Toufiq, amesema pamoja na juhudi za serikali kufungua fursa za ajira kuna
umuhimu wa kuhamasisha watanzania kuchangamkia fursa za ajira nje ya nchi.
Pia, ameshauri kufanyika kampeni maalum ya kukutana na
wakala binafsi wa ajira ili kuwajengea uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Naye, Waziri wa Nchi wa Ofisi, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye
Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ameahidi kufanyia kazi maoni ya kamati huku
akimshukuru Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua ambazo amezichukua za kukuza
uwekezaji nchini na kufungua fursa za ajira kwa watanzania.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. Patrobas
Katambi, amewahimiza watanzania wanaotaka kufanya kazi nje ya nchi kufuata
utaratibu unaotambulika na serikali ili iwe rahisi kusaidiwa wanapopata
changamoto.
Awali, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Mhandisi Cyprian Luhemeja,
amesema kitengo hicho kimetokana na kufutwa kwa Wakala wa Huduma za Ajira
(TaESA) na majukumu yake kuunganishwa chini ya Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi.
Akitoa taarifa kwa kamati, Mkurugenzi wa Kitengo hicho,
Joseph Nganga amesema miongoni mwa majukumu ya kitengo ni kuwajengea uwezo
wahitimu kushindana kwenye soko la ajira, kujenga mtazamo chanya kuhusu kazi na
kukuza maadili yanayohitajika na waajiri.
Na. Mwandishi Wetu- Dodoma
0 Maoni