Taasisi ya Marafiki wa Serengeti (Friends of Serengeti
Switzerland) wamekabidhi vifaa mbalimbali kwa Hifadhi ya Taifa Tarangire vyenye
thamani ya TZS Milioni sabini na tano (75,000,000/-) yakiwemo Mahema, miwani ya
usiku (Night Vision Goggles), kiona mbali (Binoculars), "GPS", mafuta
(Diesel) pamoja na vifaa vya kuwekea taka ngumu kwa ajili ya kufanikisha na
kuimarisha shughuli za Uhifadhi.
Makabidhiano hayo yamefanyika tarehe 24.10.2023 Makao Makuu
ya Hifadhi ya Taifa Tarangire, mkoani Manyara.
Akizungumza katika makabidhiano hayo Mwakilishi wa Taasisi
ya Marafiki wa Serengeti Switzerland, Suzan Peter Shio alisema kama taasisi
wamekuwa na mwendelezo wa kutoa vifaa mbalimbali kwa ajili ya Uhifadhi kwenye
hifadhi tofauti tofauti na leo ni Hifadhi ya Taifa Tarangire.
"Pasipo Uhifadhi hamna Utalii, nina imani vifaa hivi
vitawasaidia na kuwaongezea ari askari pale wanapokuwa katika shughuli zao za
kila siku," alisema Shio.
Akifafanua zaidi, miwani hizi za usiku (night vision
goggles) ni za kisasa, mkiwa doria usiku zitawasaidia sana kuwatambua majangili
kwa karibu na kwa urahisi, pili mafuta yatawasaidia katika doria zenu za kila
siku na shughuli za mipaka. Vifaa hivi vya kuwekea taka ngumu ni vya vituo
vyote saba ili kutunza Mazingira ya Hifadhi.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Betrice M. Kessy
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Tarangire amewashukuru Marafiki wa Serengeti kwa vifaa
vyote walivyotoa vitasaidia kuimarisha shughuli za doria na Uhifadhi.
"Nina furaha kupokea vitendea kazi hivi, kikubwa kabisa
ni miwani za kisasa za usiku (night vision goggles) kwa kuwa majangili wengi
huingia hifadhini wakati wa usiku, hii itatusaidia kuwaona na kuwakamata
kiurahisi, " alisema Kessy.
Aliongeza kuwa mafuta nayo yatasaidia sana kwenye shughuli
za doria za mchana na usiku pamoja na matengenezo ya barabara za mipakani,
kuzunguka hifadhi ili mipaka yote ionekane vizuri.
"Mipaka itaonekana bayana hivyo wananchi waheshimu
mipaka na waache vitendo vya ujangili," alisema Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Uhifadhi Kessy.
Kamishna Kessy alisema Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania
(TANAPA) linashukuru na linatambua mchango mkubwa unaotolewa na Taasisi ya
Marafiki wa Serengeti ambao tangu mwaka 1984 wamekuwa wakitekeleza miradi mingi
katika Hifadhi za Taifa Tanzania.
Na. Brigitha Kimario -Tarangire
0 Maoni