WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka madereva wa Serikali
kuwa mfano wa kuzingatia sheria zote kwa sababu kuendesha gari ya Serikali haimaanishi
wamepewa rungu la kuvunja sheria bali wanapaswa kuwa mfano wa kuzizingatia hasa
zile za usalama barabarani.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa, “ukiwa dereva wa Serikali
haimaanishi kuwa uko juu ya sheria bali kila dereva anatakiwa kuwa mfano wa kuzingatia
sheria zote. Aidha, madereva wa vyombo visivyo vya Serikali wanapaswa kujifunza
kutoka kwenu madereva wa Serikali.”
Pia, Waziri Mkuu amesema madereva hao wanapaswa kufanya kazi
kwa kufuata maadili ya taaluma ya madereva wa Serikali ambayo yanawataka
madereva hao kuzingatia na kutii sheria za usalama barabarani. “Madereva wa
Serikali hakikisheni mnakuwa kioo cha jamii.”
Ameyasema hayo jana alipofungua Kongamano la Chama cha
Madereva wa Serikali, katika Ukumbi wa Hoteli ya Morena mkoani Morogoro.
Kongamano hilo limebeba kauli mbiu isemayo; “Dereva wa Serikali bila ajali
inawezekana. Kazi iendelee”.
Akizungumzia kauli mbiu hiyo, Waziri Mkuu amesema ni kweli
inawezekana kuendesha magari ya Serikali bila kusababisha ajali iwapo kila
mmoja atatimiza wajibu wake kwa kuzingatia sheria zilizopo, hivyo amewasisitiza
madereva hao wahakikishe wanafuata sheria.
“Ninawapongeza sana kwa kuwa kaulimbiu hii pia ni
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020/2025, Ibara ya 105
(K) ambayo inailekeza Serikali kuliwezesha Jeshi la Polisi pamoja na mambo
mengine kuendelea na jukumu la kudhibiti ajali za barabarani.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali
imeshafanya jitihada kubwa katika kutatua kero za watumishi wa kada hiyo ya
udereva na bado inaendelea kuzitatua changamoto zinazojitokeza kwa kushirikiana
na Chama chao.
Amesema kuwa Serikali kupitia Wizara zenye dhamana husika
bila kuathiri shughuli na majukumu yake ya kila siku ya kiutumishi,
imebadilisha muundo wa ajira na kuondoa kigezo cha cheti cha ufundi (trade
test) katika kuwapandisha madaraja na ngazi za mshahara kwa mwaka wa fedha
uliopita.
Waziri Mkuu amewahakikishia madereva hao kuwa, Serikali ya
awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na
Serikali ya awamu ya tisa inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Ali
Mwinyi zinaendelea kutekeleza azma yake ya kulinda maslahi ya madereva wa
Serikali pamoja na kuyafanyia kazi maombi na ushauri utakaotolewa.
Naye, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewahakikishia
madereva hao kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao kupitia Chama Cha
Madereva wa Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili
kuongeza tija katika utendaji kazi Serikalini.
Pia, Waziri Bashungwa amesema suala la stahiki za madereva
linapewa msisitizo mkubwa na Serikali. Kama ilivyoelekezwa na Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, waajiri wote wahahakikishe kuwa madereva wote
wanapatiwa barua za kuthibitishwa hususan kwa wale ambao bado hawajapewa barua
hizo.
Aidha, Waziri Bashungwa amesema wizara kwa kushirikiana na
taasisi zingine za utumishi wa umma imejipanga kuhakikisha Chuo cha Taifa cha
Usafirishaji (NIT), kinaendelea kutoa mafunzo bora kwa madereva na maafisa
usafirishaji pamoja na kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Madereva wa
Serikali, Castro Nyambange pamoja na mambo mengine ameishukuru Serikali kwa
kuondoa kigezo cha cheti cha ufundi (trade test) ambacho kilikuwa
kikiwasababishia wasipande madaraja wala mishahara.
Kadhalika, Kaimu Katibu Mkuu hiyo ameiomba Serikali
kuboresha malipo ya kufanya kazi masaa ya ziada yafanyike kwa wakati na bila
upendeleo hususan madereva wa magari ya wagonjwa (Ambulance) na wanaowahudumia
madaktari na manesi wanaokuwa zamu usiku.
Lengo la kongamano hilo ni kuwawezesha madereva wa Serikali
kutoka katika mikoa, halmashauri, taasisi za umma na mashirika ya umma nchini
kujifunza masuala ya maadili ya udereva, kanuni na miongozo ya Serikali kwa
ajili ya kukuza tasnia hiyo muhimu katika kuleta mabadiliko ya kiutendaji.
0 Maoni