SERIKALI kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania (TAWA) imefadhili mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa mawili, ofisi
moja ya walimu na jumla ya madawati 30 katika shule ya msingi Usinge iliyopo
wilaya ya kaliua Mkoani Tabora
Mradi huu ambao tayari umekwishakamilika na kuanza kutumika
umegharimu kiasi cha Tsh. Millioni 50 (50,000,000/=) ambazo ni fedha
zinazotokana na bajeti ya ndani ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania
- TAWA
Akiongea na waandishi wa habari katika ziara ya ukaguzi wa
mradi huo wa maendeleo kwa jamii Oktoba 24, 2023 Afisa Habari wa TAWA Beatus
Maganja ameeleza kuwa TAWA iliona adha wanazozipata wanafunzi wa Shule ya
msingi Usinge kwa kukosa madarasa ya kutosha, ofisi ya walimu pamoja na
madawati hivyo ikaona vyema kufadhili mradi huo ili kuwapunguzia adha hizo na
kuwapa fursa wananchi kuona faida zitokanazo na shughuli za uhifadhi na umuhimu
wa uwepo wa Taasisi hiyo katika maeneo yao.
"Ifahamike kuwa changamoto kubwa katika vijiji
vinavyozunguka hifadhi ni kwamba shule nyingi zinakosa madarasa na madawati ya
kutosha lakini pia wanakosa nyenzo mbalimbali za kuwawezesha wao kuweza kusoma
katika mazingira bora," amesema Mahanja na kuongeza "Kwahiyo Mamlaka
ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania iliona vyema kufadhili miradi hii ili kuwawezesha
wananchi wanaozunguka maeneo haya kufaidi rasilimali hizi za Wanyamapori na
uhifadhi kwa ujumla."
Salma Madua Ally ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita
katika shule hiyo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr.
Samia Suluhu Hassan na Taasisi ya TAWA kwa ufadhili huo ambao ameuelezea kama
ni msaada mkubwa kwao ambao hawakuutegemea kwani umepelekea kuongeza uwezo wao
wa uelewa na ufaulu darasani.
"Nawashukuru wasimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA
pia tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea madarasa ambayo
hatukutegemea kuwa nayo, pia madarasa haya yametufanya tuweze kuwa tunafaulu na
kuwa tunaelewa vizuri," amesema mwanafunzi huyo na kuongeza "Kipindi
cha nyuma tulikuwa tunakaa darasa moja watu wengi, tulikuwa hatuwezi kuelewa kwa
urahisi lakini saizi tumegawanyishwa madarasa."
Naye Joseph Paulo mwanafunzi wa Shule hiyo ameeleza kuwa
kabla ya ujenzi wa madarasa na kufadhiliwa madawati hayo walikuwa wakikaa chini
huku wanafunzi wachache wakikalia madawati hali ambayo ilifanya nguo zao
zichafuke na kukosa umakini darasani, lakini kwa sasa wote wanakaa kwenye
madawati na kusomea kwenye vyumba vizuri vya madarasa.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Bw. Ibrahimu
Bakari Juma ameeleza kuwa shule ya Usinge ilikuwa na uhaba wa vyumba sita vya
madarasa pamoja na madawati 90 hivyo ufadhili huo uliotolewa na Serikali
kupitia TAWA umewezesha idadi ya wanafunzi 90 kukaa kwenye madawati
Aidha, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania inayoongozwa na Dr. Samia Suluhu Hassan lakini pia ameelekeza pongezi
na shukrani zake kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA kwa
ufadhili huo.
0 Maoni