Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga na Mloganzila) kwa
kushirikiana na Taasisi ya Miracle Corner World (MCW) kutoka nchini Marekeni
inatarajia kuanzisha huduma ya matibabu ya magonjwa ya kinywa na meno kwa
kutumia teknolojia ya 3D printing ambayo inarahisisha utengenezaji wa meno
bandia, vifuniko vya meno (Crown) na utengenezaji wa Taya zilizoathirika na
ajali na magonjwa mbalimbali.
Utengenezaji wa meno, vifuniko vya meno na Taya kwa kutumia
Teknolojia ya 3D Printing unatumia muda wa dakika 8 hadi kumi, tofauti na sasa
ambapo ili mtu atengenezewe jino au taya inachukua muda wa wiki mbili huku
ikihusisha michakato mbalimbali mbalimbali ya kimaabara.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya
Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi alipokutana na uongozi wa Taasisi ya MCW
kwa lengo la kujadili namna ya kuhakikisha huduma hiyo inaanzishwa haraka
katika Hospitali ya Upanga na Mloganzila.
Prof. Janabi aliangiza Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Dkt.
Rachel Mhavile na timu ya wataalamu mbalimbali kuhakikisha mchakato wa
ushirikiano huo unaharakishwa ili kufanya huduma hizi zianze kutolewa na
wananchi wanufaike.
Alisema huduma hizi zikianza zitafanya Muhimbili (Upanga
& Mloganzila) kuwa hospitali ya kwanza ya Umma nchini kutoa huduma hiyo ya
kisasa.
“Kupitia ushirikianao huu wataalamu wetu watajengewa uwezo
jambo ambalo litaendelea kuboresha huduma ya afya ya kinywa na meno na
kurahisisha huduma ya utengenezaji wa meno bandia kwa watu wanaohitaji huduma
hiyo,” alieleza Prof. Janabi
Kwa Upande wake mmoja wa viongozi wa Taasisi ya Miracle
Corner Bi Marion Bergman ameahidi kutoa ushirikiano kwa kuwajengea uwezo
wataalamu wa Muhimbili ili waweze kutoa huduma hiyo kwa ufanisi zaidi.
0 Maoni