WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa, amewataka wananchi kwenye
maeneo mbalimbali nchini washiriki katika michezo kwa kuwa michezo ni ajira,
uchumi na huimarisha afya.
“Tunapa faida nyingi kwa kufanya michezo, tushiriki katika
michezo pamoja na kukimbia riadha kwa kuongeza vipaji tulivyonavyo kwani
tukishindana tunapata na zawadi. Michezo ni uchumi. “
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumamosi, Septemba
9, 2023) baada ya kuzindua Ruangwa Marathon katika kiwanja cha Kilimahewa,
wilayani Ruangwa Lindi.
Aidha, Waziri Mkuu amesema amemshukuru Rais Mheshimiwa Samia
Suluhu Hassan kwa maboresho makubwa aliyoyafanya katika sekta ya afya nchini
ikiwemo na wilaya ya Ruangwa.
Amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika maeneo ya
kutolea huduma za afya kwa kujenga zahanati, vituo vya afyfa na hospitali ya
wilaya ambayo inavifaa tiba vya kisasa.
Mbio hizo za hisani ambazo zimefanyika kwa mara ya kwanza
wilayani Ruangwa zimehudhuriwa na wanariadha mbalimbali wanaoliwakilisha Taifa
katika mashindano ya mbio za kimataifa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Molel
amesema mbio hizo za marathon ni nzuri kwa sababu mazoezi yanasaidia katika
kupambana na magonjwa yasiyoambukiza.
Dkt. Molel amemshukuru Waziri Mkuu kwa kukubali kuwa mgeni
rasmi katika mbio hizo za hisani zilizokuwa na lengo la kukusanya fedha kwa
ajili ya kununulia vifaa tiba wilayani Ruangwa.
Pia, Dkt. Molel ameishukuru Serikali kwa kuboresha huduma za
afya ambapo kwasasa asilimia 97 ya wagonjwa waliokuwa wanapelekwa nje ya nchi
kwa matibabu wanatibiwa nchini.
0 Maoni