Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo ameinadi
Minada ya Madini kwa Wafanyabiashara Wakubwa nchini Thailand ikiwa ni
maandalizi ya Serikali kuirejesha tena baada ya kuifungia kwa muda.
Mbibo amewafahamisha wafanyabiashara hao kwenye Semina
iliyofanyika Septemba 8, 2023 jijini Bangkok katika maonesho ya 68
yanayoendelea nchini humo ambapo semina hiyo imejadili fursa zilizoko katika
tasnia ndogo ya madini ya vito na usonara kwa nchi za Mashariki ya Kati ambazo
ni miongoni mwa nchi zilizobobea kwenye shughuli za uongezaji thamani madini,
nchi wanunuzi na watumiaji wakubwa wa madini ya vito na usonara duniani.
Ameieleza hadhira hiyo kuwa, Tanzania ikiwa mzalishaji
mkubwa wa madini ya vito na wao kama wafanyabiashara wakubwa wa madini hayo,
wanayo nafasi kubwa ya kushiriki moja kwa moja katika minada ya madini ambayo
inatarajiwa kurejeshwa tena mapema mwaka 2024, ikiwemo kushirikiana na Tanzania
katika nyanja mbalimbali za kibiashara, uongezaji thamani madini na
kushirikiana katika kuongeza ujuzi kwa
watanzania waweze kuzalisha bidhaa zenye ubora na zinazokidhi viwango vya
kimataifa kwenye soko la dunia na hatimaye kuchochea hamasa kwa watanzania
kujikita katika eneo hilo.
Hivi sasa Serikali iko katika hatua za mwisho za mchakato wa
kuwasilisha mapendekezo ya maboresho ya Sheria na Kanuni ili kuwezesha maonesho
na minada ya vito kurejea ikiwemo marekebisho ya Kanuni za Eneo Tengefu la
Mirerani za Mwaka 2021 ambazo zilizuia kuuzwa kwa madini ya Tanzanite nje ya
Mirerani.
Kufanyika kwa minada hiyo kuna manufaa makubwa kwa Tanzania ambapo
pamoja na mambo mengine itasaidia kuyatambulisha madini yanayozalishwa nchini,
kuchangia fedha za kigeni, kuyaongezea thamani, kuongeza tija katika sekta ya
madini na kuwahamasisha wauzaji na wanunuzi wakubwa wa madini duniani kununua
moja kwa moja kutoka nchini.
Aidha, Mbibo ametumia jukwaa hilo baada ya Tanzania kupata
heshima ya kuzungumza katika semina hiyo ambapo amewakaribisha kushiriki katika
Jukwaa la Kimataifa la Uwekezaji katika Sekta ya Madini linalotarajiwa
kufanyika tarehe 25 na 26 mwezi Oktoba, 2023 jijini Dar es Salaam.
Ameongeza kwamba, jukwaa hilo litawapa nafasi ya kukutana na
wauzaji, kufahamu fursa za kibiashara zilizopo nchini, kujenga mahusiano ya kibiashara
na wadau kutoka pande mbalimbali duniani na kufahamu kwa kina kuhusu utajiri wa
rasilimali madini uliopo Tanzania ambayo ni miongoni mwa nchi wazalishaji
wakubwa wa madini ya vito ambapo nchi husika ni walaji.
Katika hatua nyingine, katika mazungumzo yake na wadau hao,
amesema wameonesha nia ya kushirikiana na Serikali kuhusu namna ya kuendesha
minada hiyo ili kuifanya kuwa na sura ya kimataifa na hivyo wameiomba Wizara
iharakishe mchakato wa kurejeshwa kwake.
"Wafanyabiashara
hawa pia wameonesha utayari wa kushirikiana na sekta binafsi kuendeleza Sekta
ya Madini nchini katika eneo hilo,’’ amesema Mbibo.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kituo cha Jemolojia Tanzania
(TGC) Daniel Kidesheni ametoa wito kwa vijana wa Tanzania kuigeukia tasnia
ndogo ya uongezaji thamani madini kutokana na fursa nyingi za kibiashara na
ajira zilizopo katika eneo hilo kutokana na utajiri mwingi wa madini ambao nchi
ya Tanzania imebarikiwa kuwa nao.
Ameongeza kwamba, semina hiyo imeongeza ujuzi kwa Kituo
hicho kuona namna bora ya kuwaendeleza vijana wa kitanzania kupitia mafunzo
yanayotolewa, matumizi ya teknolojia za kisasa na namna ambavyo ukanda huo
ulivyofanikiwa kurithisha taaluma hiyo kwa vizazi na vizazi
Shughuli za uongezaji thamani madini ya vito ni biashara
ambayo imeshamiri kwa kiasi kikubwa katika eneo la nchi zilizopo Mashariki ya
Kati ikiwemo nchi ya Thailand ambayo ni maarufu katika utengenezaji wa vito vya
rangi za kuvutia na imekuwa ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato kwa nchi
hizo ikiwemo ajira.
Semina hiyo imehusisha wadau wa madini ambao ni wabobezi katika
biashara ya vito, shughuli za uongezaji thamani madini ambapo wamejadili
masuala mbalimbali ikiwemo namna ya kuongeza utaalam zaidi katika eneo hilo.
0 Maoni