Waziri wa Nchi, Ofisi Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, Mhe.George Simbachawene
ameutaka Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kuacha kulitumia gari la
kubebea wagonjwa (Ambulance) la Kituo cha Afya cha Rudi kwa matumizi mengine
badala yake gari hilo litumike kwa lengo lililokusudiwa ili kusaidia kupunguza
vifo vya akina mama wajawazito na wagonjwa wengine pindi linapohitajika.
Amesema ni aibu kuona gari ya kubebea wagonjwa likitumika
kwa ajili ya kufanyia mambo mengine huku kusudio la msingi wa gari hilo llikiwa
limeachwa huku akina mama wajawazito na wagonjwa wengine mahututi wakihatarisha
maisha yao.
Mhe. Simbachawene ameyasema hayo wakati akizungumza na
wananchi wa Kata ya Rudi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Shule ya
Msingi ya Chilendu, Jimbo la Kibakwe katika Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma,
ikiwa ni ziara yake ya kimkakati ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha
Mapinduzi
Amesema malalamiko ya wananchi walio katika hali duni ni
mengi kuhusu matumizi ya gari hilo, kusudio la gari hili ilikuwa ni kuwasaidia
wagonjwa walioshindwa kutibiwa katika Kituo hicho cha afya waweze kukimbizwa
katika Hospitali ya juu zaidi ili kuokoa maisha yao lakini muda mwingi gari
hilo limekuwa likitumika kwa shughuli zingine katika Halmashauri ya Mpwapwa
ambako ni mbali na kituo kilipo.
"Unakutana na gari la kubebea Wagonjwa limebeba maofisa
wa Halmashauri ilhali huku wagonjwa wanaohitaji kusafirishwa kwa matibabu zaidi
wakilazimika kukodi gari kutoka kwa watu binafsi, jambo hili halikubaliki,"
amesema Mhe.Simbachawene.
Aidha, Mhe.Simbachawene ametaka gari hilo liwepo saa 24
katika Kituo hicho cha Afya badala ya kuliweka katika ofisi za Halmashauri ya
Wilaya Mpwapwa kwa madai kuwa hakuna wagonjwa wanaolihitaji.
Ameutaka Uongozi huo wa Halmashauri kujitathmini kama wapo
pale kwa ajili ya kuwahudumia wananchi kwani haiwezekani wananchi wakiachwa
wanataabika na muda mwingine hupoteza maisha ilhali gari lipo ila linatumika
kwa matumizi yasiyo yake.
Kwa mujibu wa wananchi, licha ya kujitahidi kutumia nguvu
zao kujenga sehemu maalum ya kuhifadhia gari hilo la wagonjwa katika kituo
hicho cha afya lakini gari hilo muda mwingi limekuwa halikai hapo.
Katika hatua nyingine, Mhe.Simbachawene ametoa wito kwa
akina mama wajawazito kuwahi katika vituo vya afya mara waonapo dalili za
kuanza kwa uchungu ili kuepuka vifo visivyo vya lazima huku akiwasihi manesi
kuwahudumia wagonjwa kwa upendo kama viapo vyao vinavyowataka
0 Maoni