WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza Afisa Mfawidhi wa Kituo
cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) cha Mutukula, Bw. Feisal Nassoro na
wenzake watatu warudishwe makao makuu mara moja na kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Watumishi wengine ni Bw. Gerald Mabula, Bw. George Mwakitalu
na Bw. Emmanuel Malima ambao ni maafisa mapato wa TRA.
Ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Septemba 23, 2023) wakati
akizungumza na wafanyabiashara na wakazi wa Mutukula mara ya kufanya ukaguzi
kwenye Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani (One Stop Border Post) cha Mutukula,
wilayani Missenyi mkoani Kagera.
“Watumishi hawa wanne warudishwe makao makuu kwa sababu ya
kudharau mamlaka na kuikosesha Serikali mapato. Ukaguzi ulifanywa na Kamati ya
Usalama ya Wilaya wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya lakini walipewa dharau kana
kwamba hiki ni chombo kilicho juu ya sheria.”
“Mkuu wa Wilaya ni mkuu na msimamizi wa shughuli za Serikali
ndani ya wilaya yake. Anapotaka taarifa anastahili apatiwe. Uongozi wa mkoa
ulipokuja nao pia waliambulia dharau. Hatuwezi kukubali kuona mtumishi wa umma
anafanya mambo ya hovyo halafu sisi tunamuacha,” amesisitiza.
Waziri Mkuu amesema wakati Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan akiwa kwenye ziara ya mikoa ya Kusini alisisitiza kuwa mtumishi ambaye
hatekelezi majukumu yake, sisi hatutamvumilia. “Ni lazima watumishi tuwe na
nidhamu ya kazi, ni lazima tuheshimu mamlaka,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wakazi wa
Mutukula wachangamkie fursa ya uwepo wao mpakani na kuimarisha biashara zao.
“Mutukula ni mji wa kibiashara na unakua kwa kasi sana. Hapa
Mutukula ni sawa na Tunduma, Kasumulo, Sirari na Namanga. Lazima mji huu uwe
unakimbiliwa na watu wa nje na wa ndani. Hivyo Halmashauri ya Wilaya ijipange
ijenge kituo kizuri cha mabasi ili watu wakija wapate mahali pa kupumzikia.”
Waziri Mkuu yuko mkoani Kagera kwa ziara ya siku tatu.
0 Maoni