Lori lagonga gari la abiria na kuua watu 9, wengine 23 wajeruhiwa

 

Watu tisa wamekufa na wengine 23 kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea kwenye mteremko wa Iwambi Wilaya ya Mbeya Vijijini Mkoani Mbeya baada gari lao kugongwa nyuma na lori la mafuta.

Ajali hiyo iliyotokea jana majira ya saa 11:30 jioni, ilihusisha lori aina ya Howo lenye usajili namba BCE 9384/ABX 8675 la Kampuni ya Horn Afric Motors Ltd ya Zambia na Mitsubishi ROSA namba T 636 DQY iliyokuwa ikitokea Mbeya kuelekea Mbalizi.

Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya ACP Benjamin Kuzaga amesema chanzo cha ajali ni dereva wa lori kushindwa kulimudu gari lake kwenye mteremko mkali na kwenda kuligonga kwa nyuma gari la abiria. Dereva wa lori amekamatwa na atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Kamanda Kuzaga amesema kati ya watu waliokufa wanaume ni watano, wanawake ni wanne, ambapo kwa upande wa majeruhi wanaume 13 na wanawake 10. Majeruhi wanaendelea kutibiwa Hospitali Teule ya Ifisi iliyopo Mji Mdogo wa Mbalizi na wengine wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa madereva ambao wanapita katika Mkoa wa Mbeya kwenye milima na miteremko mikali kuhakikisha wanakagua magari yao kabla ya kuanza safari na wamiliki wa magari wasiruhusu magari yao kuendeshwa na madereva hao ili kuepusha ajali.

Chapisha Maoni

0 Maoni