Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Mhe. Vincent Mashinji amesema
uwepo wa wanyama Faru katika Hifadhi ya Taifa Serengeti umechangia kuongezeka
kwa idadi ya watalii. Ongezeko la wanyama hao ambao ni kivutio kwa watalii wa
ndani na nje limechangiwa na juhudi kubwa za ulinzi zinazofanywa na maafisa na
askari wa TANAPA waliojitolea kwa jasho na damu kuhakikisha wanyama hawa adimu
wanaendelea kuwepo.
Dkt. Mashinji ameyasema hayo hapo jana ikiwa ni maadhimisho
ya siku ya Faru duniani yaliyofanyika Fort Ikoma wilayani Serengeti kwa
kushiriki mbio fupi kwa ajili ya kuadhimisha siku hii. Na kusema, "Nimefurahi
kuambiwa kuwa wanyama hawa adimu idadi yao inaongezeka mwaka hadi mwaka,
ongezeko la wanyama hawa limeendelea kuvuta watalii wengi sana wa ndani na nje
ya mipaka ya Tanzania. Niwahakikishie kama Mkuu wa wilaya hii ya Serengeti
nitashirikiana na TANAPA kukilinda kizazi hiki cha Faru kisitoweke".
Aidha, nawapongeza sana maafisa na askari kwa kuwatunza Faru
hawa, kwa kuwa idadi inaendelea kuongezeka niwaombe kushirikiana na jamii
inayozunguka hifadhi hii, watoe taarifa pale wanapowaona wakiwa nje ya maeneo
ya asili ili wasiuwawe na majangili wasioutakia mema uhifadhi.
Hata hivyo Dkt. Mashinji aliwashauri TANAPA kuona kama kuna
uwezekano wa wanyama hao pia, kuongezwa na kuhifadhiwa katika Hifadhi za Taifa
Burigi-Chato, Arusha na Nyerere ili watalii wenye shauku ya kuwaona Faru wawe
na machaguo mengi zaidi badala ya Serengeti na Mkomazi kama ilivyo sasa.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Albert Mziray akimkaribisha
mkuu wa wilaya hiyo, alitoa pongezi kwa wawekezaji kwa mchango wao mkubwa
katika kufanikisha kazi hii adhimu ya Uhifadhi na utunzaji wa Faru.
" Nichukue nafasi hii kuwapongeza Frankfurt, WWF,
Friends of Serengeti na majirani zetu TAWA kwa kuja kwenye maadhimisho haya.
Pia kwa mchango mkubwa mnaoutoa katika kufanikisha utunzaji wa Faru hawa na
shughuli zote za Uhifadhi kwa ujumla".
Akifafanua kwa niaba ya Mratibu wa Faru Taifa Mhifadhi Mkuu
Emmanuel Kaaya amesisitiza tuendelee kuweka jitihada katika ulinzi wa Faru na
ulinzi huu unaendelea kuimarishwa ili kutimiza malengo ya Uhifadhi wa FARU
haswa katika kutekeleza mkakati wa FARU Taifa.
Aidha, Kaaya alisema, “tutawapa tuzo washindi wa mbio za
asubuhi pamoja na watumishi waliojitolea usiku na mchana kuwahifadhi Faru kwa
mwaka huu 2023 tunafanya hivi ili kuenzi na kuheshimu mchango wenu”.
Maadhimisho haya yamefanyika katika Hifadhi ya Taifa
Serengeti kwa kuanza na mbio zilizohamasisha utunzaji wa Faru na kuongozwa na
kauli mbiu inayosema
"Tuwalinde Faru dhidi ya Ujangili ili tuongeze idadi
yao."
Na. Brigitha Kimario - Serengeti
0 Maoni