Wizara ya Afya kwa Kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI
hadi sasa imeweza kusambaza vifaa vya mtu kujipima mwenyewe maambukizi ya
Virusi vya UKIMWI zaidi ya Mil. 1.6 kuanzia Mwaka 2021 nchini Tanzania.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo
kwenye kilele cha Mdahalo wa Kitaifa wa Baraza la Taifa la watu wanaoishi na
Virusi vya UKIMWI Tanzania (NACOPHA) uliofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya
Kikwete Jijini Dodoma ambapo Mgeni rasmi alikua ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.
Waziri Ummy amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi
ya Rais TAMISEMI itaendelea kuongeza nguvu za kusambaza vifaa hivyo vya watu
kujipima wenyewe Virusi vya UKIMWI ili kuweza kutambua hali zao wenyewe na kwa
haraka kuhusu ugonjwa huo.
Waziri Ummy amebainisha kuwa Serikali ya Rais Samia Suluhu
Hassan imeendelea kupanua wigo wa vituo vya kupima na kutoa huduma za matunzo
(CTC) kwa watu wenye UKIMWI ambapo hadi sasa tuna vituo 8,529.
“Nitoe rai kwa watu wote wanaoishi na VVU kuzingatia
matumizi sahihi na endelevu ya dawa za kufubaza Virusi vya UKIMWI ili kuweza
kujilinda wao wenyewe lakini pia kuwalinda wengine,” amesisitiza Waziri Ummy.
Pia, Waziri Ummy amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya
pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kutoa huduma za kupima, tiba na
matunzo kwa watu wanaoishi na VVU hapa nchini ili vituo vyote vinavyotoa huduma
za Afya viwe pia vituo vya kupima na kutoa matunzo (CTC) kwa 95% ifikapo Mwaka
2025.
Aidha, Waziri Ummy amesema chini ya uongozi mahiri wa Rais
Dkt. Samia, Serikali itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vitendanishi
kwaajili ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI na kuendelea kufuatilia taarifa
zote kuhusu uwepo wa dawa mpya ambazo ni bora zaidi.
Mwisho, Waziri Ummy amelipongeza Baraza la Taifa la watu
wanaoishi na VVU Tanzania (NACOPHA) kwa kuanzaa mdahalo wa kuadhimisha Miaka
20, “Sekta ya Afya inatambua mchango wao mkubwa katika mapambano dhidi ya
UKIMWI”.
0 Maoni