WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza wataalamu wa mifumo na TEHAMA, wabuni programu tumizi ya kuweza kutambua risiti halali na zisizo halali ili kujihakikishia kuwa mapato yote yanayokusanywa yanaingia Serikalini.
Kadhalika, amewataka waweke utaratibu wa kufanya kaguzi za
mashine za “PoS” ili kubaini kama kuna ukiukwaji wowote unaofanyika sambamba na
kuwa na utaratibu endelevu wa ufuatiliaji na mfumo wa usalama maalum wa utunzaji
taarifa (back-up).
Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Septemba 8, 2023) wakati wa
kuahirisha Mkutano Wa 12 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bungeni
jijini Dodoma.
“Niwakumbushe watumishi wa umma kuwa bado tunalo jukumu la
kuendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyosisitiza juu ya usimamizi
wa ukusanyaji mapato kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa wakati akifunga
mafunzo ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa mjini Kibaha,” alisema
Majaliwa.
Mheshimiwa Majaliwa amesema, Serikali iliunda mfumo mpya wa
ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri ujulikanao kama TAUSI ili
kupunguza urasimu uliokuwepo kwenye ukusanyaji wa mapato. “Mfumo huu mpya ni wa
kidijitali na humrahisishia mfanyabiashara kufanya malipo ya Halmashauri kwa
njia ya mtandao kwa kutumia simu yake ya kiganjani au kompyuta”
“Mfumo huu umelenga kumsaidia mteja kujihudumia mwenyewe,
hali ambayo haimlazimu tena kwenda ofisi za halmashauri kuomba au kulipia tozo,
ushuru, leseni, faini au vibali mbalimbali. Badala yake anaweza kufanya
mwenyewe kupitia dirisha la mteja au Taxpayer Portal,” alisema Majaliwa.
“Nipende kuwasisitiza wafanyabiashara na watoa huduma watoe
risiti halali kupitia mashine za kielektroniki (EFDs) wakati wa mauziano ya
bidhaa au utoaji wa huduma kwa wateja. Kwa upande wa wateja, niwakumbushe kuwa
ni wajibu wao kudai risiti yenye thamani halisi ya fedha walizotoa,” alisema
Majaliwa.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa, amewataka waajiri wachukue hatua
za kuimarisha mifumo ya kuwalinda wafanyakazi wao dhidi ya vihatarishi
vilivyomo katika maeneo yao ya kazi.
Hatua hizo ni pamoja na kuwa na mwongozo wa Usalama na Afya
Mahali pa Kazi, kufanya tathmini ya vihatarishi mahali pa kazi, kuhakikisha
wafanyakazi wao wanapimwa afya ili kubaini athari ya vihatarishi kwa mfanyakazi
na kuhakikisha maeneo yao yanafanyiwa kaguzi za usalama na afya ili kuwalinda
wafanyakazi na kulinda uwekezaji wao.
“Nitoe wito kwa watumishi wa OSHA wawe waadilifu
wanapoendesha mazoezi ya ukaguzi mahali pa kazi na kuchukua vipimo vya
wafanyakazi,” alisema Majaliwa.
Pia amewataka, Wafanyakazi wahakikishe wanazingatia taratibu
na miongozo ya kujilinda dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kusababisha ajali au
magonjwa wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ameagiza
watendaji wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kuongeza wigo wa kutoa elimu kwa
wafanyakazi ili watambue huduma zinazotolewa na mfuko huo. Vilevile, waajiri
watumie ipasavyo mifumo ya TEHAMA kupata huduma, kujisajili na kuwasilisha kwa
wakati michango katika mfuko huo.
0 Maoni