Askari wahifadhi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania (TAWA) septemba 11, 2023 walifanikiwa kumuokoa mtoto wa tembo
anayekadiriwa kuwa na umri wa wiki nne (4) aliyezama katika shimo lenye matope
katika Kijiji cha Kwamsanja kilichopo kata ya kibindu halmashauri ya Chalinze
jirani na Pori la Akiba Wamimbiki.
Taarifa za Mtoto huyo wa tembo aliyetelekezwa na kundi lake
kutumbukia shimoni zilitolewa na raia mwema aitwaye Manase Thomas Baha mkazi wa
Kijiji cha Kwamsanja na kumlazimu Kamanda wa Pori la Akiba Wamimbiki Emmanuel
Lalashe kutuma timu ya askari wanne (4) walioshirikiana na askari wa Jeshi la
Akiba (migambo) sita (6) kwa ajili ya zoezi zima la kumuokoa mtoto huyo wa
tembo.
Akizungumza baada ya zoezi la uokoaji, Kamanda Emmanuel
Lalashe aliwashukuru wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi ya Wamimbiki kwa
ushirikiano wanaoutoa katika kulinda rasilimali za Nchi yetu zilizopo katika
hifadhi hiyo hususan rasilimali Wanyamapori ambazo ni chachu ya shughuli za
Utalii na Pato la Nchi.
Mahusiano mazuri yaliyojengwa kati ya wahifadhi wa hifadhi
ya Wamimbiki na wananchi wanaoishi vijiji Jirani na hifadhi hiyo umekuwa na
manufaa makubwa siku za hivi karibuni kwani wananchi wamekuwa wakitoa
ushirikiano mkubwa katika shughuli za uhifadhi.
Na. Beatus Maganja- TAWA
0 Maoni