Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na
Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis ameitaka jamii kutokukaa kimya na
kunyamazia vitendo vya ukatili vinavyotokea ili kuwa na Jamii iliyo salama hasa
kwa Wanawake na Watoto.
Mhe. Mwanaidi ameyasema hayo wakati wa ziara yake mkoani
Geita jana iliyolenga kufuatilia utekelezaji wa sera na mipango mbalimbali ya
wizara katika Mamlaka ya Mikoa na Serikali za Mitaa nchini.
"Nimefika katika Mkoa huu wa Geita nimepokea taarifa ya
Mkoa nimeona masuala ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto yameshamiri, jumla
ya mashauri 625 kwa watu wazima na mashauri 133 ya vitendo dhidi ya watoto
yameripotiwa, sasa tusikae kimya tupaze sauti tutokomeze ukatili,” amesema Mhe.
Naibu Waziri.
Aidha, amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya
Jamii kuwasikiliza wananchi katika maeneo yao ili kuwasaidia kutatua changamoto
mbalimbali wanazokabilia nazo katika jamii hasa za upatikitanaji wa fursa za
kiuchumi na ukatili wa kijinsia.
"Ndugu zangu Maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya
Jamii Rais Samia Suluhu Hassan ameiunda Wizara hii muhimu mtusaidie kuwafikia
wananchi kutatua changamoto zao, tuwasaidie wananchi tuwasikilize," amesisitiza
Mhe. Naibu Waziri.
Wakati huo huo Mhe. Naibu Waziri Mwanaidi amepokea taarifa
ya Utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na
Watoto (MTAKUWWA) katika Kata ya Nyamigota na amewasihi wajumbe wa kamati ya
MTAKUWWA kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii ili wawe na uwezo wa kutoa taarifa
za vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kuilinda jamii.
Pia Naibu Waziri Mwanaidi ametembelea Kikundi cha Manyuki
Company Grading Rice killichopo Mamlaka ya Mji mdogo wa Katoro Halmashauri ya
Wilaya ya Geita na kuwataka Wanawake kujiunga katika vikundi vya kiuchumi ili
waweze kupata fursa mbalimbali za kupata mikopo kwaajili ya kupata mitaji na
masoko ya bidhaa wanazozalisha katika vikundi vyao.
Kwa upande Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Geita Karia
Rajab Magaro amemuhakikishia Mhe. Naibu Waziri Mwanaidi kuratibu masuala yote
ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii na kuhakikisha Maafisa wa kada hizo
wanawafikia wananchi kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza
katika jamii.
"Nakuhakikishia Mhe. Naibu Waziri, tutayasimamamia
masuala yote ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii katika Halmashauri ya
Wilaya ya Geita ili wananchi waweze kupata huduma na namna za kupambana na
changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii yetu," amesema Magaro.
Pia Naibu Waziri Mwanaidi ameihamasisha Jamii kutumia fursa
ya Kituo cha Huduma kwa Mteja Jamii Call Center kilicho katika Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kupiga namba
026-2160250 au 0734 986 503 kwa elimu, msaada na changamoto mbalimbali za
wananchi.
Nao baadhi ya Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita
wameishukuru Wizara kwa kufuatilia utekelezaji wa Afua mbalimbali na kuiomba
Serikali kuendelea kuongeza nguvu katika kuihudumia Jamii hasa kuongeza idadi
ya Maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii katika Kata na Vijiji.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na
Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis yupo katika ziara mkoani Geita
kufuatilia utekelezaji wa Sera, na Mipango mbalimbali ya Wizara.
Na, WMJJWM- Geita
0 Maoni