Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.
Dk. Hussein Ali Mwinyi ameondoka Zanzibar kuelekea Havana, Cuba kumwakilisha
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika
Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kundi la 77 na China (G77+ China)
utakaofanyika tarehe 15 hadi 16 Septemba 2023.
Mkutano huo unalenga kukutanisha Mataifa yanayoendelea
(Developing Countries) ili kujadili changamoto zinazoikabili dunia hasa baada
ya kuathirika na UVIKO-19 na migogoro inayoendelea duniani pamoja na vikwazo
mbalimbali vya kiuchumi.
Hivyo, mkutano huo utajikita zaidi katika kutafuta namna
bora ya kujenga ustahimilivu kupitia maendeleo ya sayansi na teknolojia na ubunifu
ili kundi la G77 na China liweze kufikia malengo yake kwa pamoja.
Mkutano huu utaongozwa na kaulimbiu isemayo “Current
Development Challenges: The Role of Science, Technology and Innovation”.
Rais Dk. Mwinyi anatarajiwa kuhutubia mkutano huo na kuelezea
vipaumbele vya Tanzania, pamoja na hatua zilizochukuliwa kukuza tafiti na
kuimarisha matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu (STI) katika kuleta
mapinduzi ya kiuchumi.
0 Maoni