Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema Tanzania
ni miongoni mwa nchi zenye rasilimali madini kwa wingi yakiwemo Madini Mkakati
ambayo mahitaji yake yanazidi kuongezeka kutokana na kutumika kuzalisha aina
tofauti za vyanzo vya nishati na teknolojia zinazohitaji aina mbalimbali za
madini mkakati kama vile Lithiamu, Nikeli, Kobalti, Manganese na Grafiti.
Dkt. Kiruswa ameyasema hayo jana jijini Paris nchini
Ufaransa wakati akihutubia Mkutano wa Kilele wa Usalama wa Madini Mkakati ambao
umejadili masuala muhimu kuhusu madini hayo, kubadilishana uzoefu pamoja na
kujadili namna ya kushiriki katika kuchochea usimamizi na usambazaji endelevu
wa madini hayo
Alisema kuwa kutokana na mwelekeo wa sasa teknolojia,
zinahitaji aina mbalimbali za madini mkakati na kwamba, nchini Tanzania madini
hayo yanapatikana kwa wingi.
“Ndugu Washiriki, mengi ya madini mkakati yanayohitajika kwa
mabadiliko ya nishati safi yanapatikana kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania. Hizi ni pamoja na rasilimali muhimu ya
Grafiti, Nikeli, Kobalti, Lithiamu, Vipengee Adimu vya Dunia (Rare Earth
Elements [REE]), Shaba, Manganese, Zinki na Alumini,” alisema Dkt. Kiruswa.
Aidha, Dkt. Kiruswa alisema kuwa kutokana na uwepo wa
rasilimali hizo Tanzania ni miongoni mwa wadau muhimu katika Mkakati wa Mpito
wa Nishati Safi kutokana na kuwa na Rasilimali Madini muhimu na Mkakati ya aina
mbalimbali kwa kiasi kikubwa.
Sambamba na hilo, Dkt. Kiruswa aliueleza mkutano huo kuwa,
miongoni mwa masuala yanayohitaji mkakati wa pamoja wa kimataifa, ni pamoja na
namna bora ya ugavi wa madini hayo, uboreshaji wa uwazi wa masoko, kuongeza
kasi ya teknolojia za uvumbuzi na uchakataji na kukuza mazoea ya maendeleo
endelevu na yenye uwajibikaji.
Aidha, alitumia jukwaa hilo kuwakaribisha wawekezaji
kuwekeza nchini na kuongeza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi barani Afrika
ambazo zina amani na utulivu mkubwa kisiasa.
“Tanzania imeunganishwa vyema na mitandao mizuri ya barabara
inayofanya mikoa na wilaya zote kufikika.
Faida nyingine kubwa ya kuwekeza nchini Tanzania ni uwepo wa mfumo ujao
wa reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR) ambao unaendelea kujengwa kuanzia
Bandari ya Dar es salaam hadi katika nchi jirani zisizo na bandari zikiwemo
Rwanda, Zambia, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)” aliongeza
Dkt. Kiruswa.
Mbali na Naibu Waziri, wengine walioshiriki kutoka Wizara ya
Madini ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo, Kamishna Msaidizi
wa Madini sehemu ya Uendelezaji Migodi kutoka Wizara ya Madini, Terence Ngole,
Kaimu Mkurugenzi wa Kanzidata kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini
Tanzania (GST) Hafsa Seif.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mawaziri, Wafanyabiashara,
Wawekezaji, taasisi za kimataifa na taasisi za kiraia kutoka nchi tofauti
Ulimwenguni.
Katika hatua nyingine Ujumbe huo wa Tanzania ulipata nafasi
ya kuzungumza na wadau wengine wa Sekta ya Madini kutoka mataifa mbalimbali
ikiwemo India ambapo ulizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kabir
ambayo ni sehemu ya Shirika la Madini la Taifa Nchini India, lengo likiwa ni
kuona namna nzuri ya kuanzisha ushirikiano wa kikazi na kubadilishana ujuzi
kwenye Sekta ya Madini.
0 Maoni