Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga amewapa saa sita
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuirejesha katika hali ya kawaida ya
uzalishaji mitambo iliyopata hitilafu katika kituo cha Ubungo I.
Kapinga amesema hayo wakati wa ziara ya kukagua hali ya
uzalishaji wa umeme katika Vituo vya Kupoza na Kusambaza Umeme vya Ubungo I na
Ubungo II ili kuona hali ya uzalishaji katika vituo hivyo, Septemba 29, 2023
jijini Dar es Salaam.
Aliwaeleza kuwa, kutokana na changamoto ya upatikanaji wa
umeme nchini, ni vyema TANESCO wakaweka mpango wa kufanya marekebisho ya muda
mfupi, wakati na muda mrefu katika mitambo, na marekebisho hayo yafanyike kwa
wakati na muda sahihi ili kutimiza azma ya Serikali ya kuhakikisha kuwa
watanzania wanapata umeme wa uhakika wakati wote.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan, ameshatoa maelekezo kuwa matengenezo yafanyike na ndani ya miezi
sita yakamilike, sisi kama Wizara tunasimamia na kuhakikisha kuwa kila mashine
ambayo inatakiwa kufanyiwa marekebisho inafanyiwa marekebisho hayo na
yanamilika kwa wakati,” alisema Kapinga.
Kapinga alifafanua kuwa mashine zenye hitilafu husababisha
upungufu katika usambazaji wa umeme na hivyo watumiaji kuilaumu Serikali juu ya
hali hiyo.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri huyo amekagua kituo cha
Ubungo II chenye mitambo mitatu ambapo kati ya hiyo uko kwenye matengenezo na
Katika kituo cha ubungo I chenye mashine 12, ambapo sita zinafanya kazi na
nyingine ziko kwenye matengenezo.
Na. Zuena Msuya- DSM
0 Maoni