Kufuatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya
Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan
Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila itafanya huduma ya kibingwa na Bobezi
ya upandikizaji figo kwa wagonjwa watano kuanzia Oktoba 2 hadi 6, 2023.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Upasuaji,
Dkt. Godlove Mfuko upandikizaji huo ni wa kisasa ambapo utahusisha kutoa figo
kutoka kwa mchangiaji kwa kutumia njia matundu (Hand Assisted Laparascopic
Nephrectomy), utaalamu ambao kwa hapa nchini unafanyika MNH-Mloganzila pekee
ukilinganisha na hospitali zingine ambazo humfanyia upasuaji mchangiaji.
Dkt. Mfuko ameongeza kuwa upandikizaji huu unaohusisha kutoa
figo kutoka kwa mchangiaji kwa kutumia matundu madogo unamsaidia mchangiaji
kutokua na kovu kubwa, kupona mapema na kurudi katika majukumu yake mapema
zaidi ukilinganisha na upandikizaji uliozoeleka ambao mchangiaji hufanyiwa
upasuaji.
“Hii ni mara ya pili kwa hospitali yetu kupandikiza figo kwa
njia ya matundu, hapo awali tuliwafanyia wagonjwa watatu ambao kwa sasa
wanaendelea vizuri na mpango wetu ni kufanya upandikizaji wa aina hii kila
mwezi,” amebainisha Dkt. Mfuko.
Dkt. Mfuko amebainisha kuwa upandikizaji huu umewezekana
kutokana na Serikali kuwajengea uwezo wataalamu wetu wa ndani, kununua vifaa
tiba na kujenga miundombinu wezesheshi katika kutoa huduma za upandikizaji figo
MNH Mloganzila jambo ambalo limesaidia kupunguza gharama kwa wagonjwa kwa zaidi
ya asilimia 50 endapo wagonjwa hao wangepelekwa nje ya nchi kwa upandikizaji.
Upandikizaji huu wa figo unafanywa na wataalamu wa ndani kwa
kushirikiana na mtaalamu kutoka nchini Korea Kusini Prof. Park Kwan Tae chini
ya Taasisi ya Korea Foundation for International Health Care (KOFIH).
0 Maoni