WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wahitimu 521 wa
mafunzo ya Kozi Na. 01/2023 wakatumie vema ujuzi na maarifa waliyoyapata katika
kudhibiti vitendo vya uhalifu hususan maeneo ya vipenyo, vituo na mipakani.
Mhe. Majaliwa ametoa wito huo jana alipofunga mafunzo hayo
kwa askari wa Uhamiaji katika Chuo cha Mafunzo ya Uhamiaji cha Raphael Kubaga,
Wilayani Mkinga, katika Mkoa wa Tanga.
Waziri Mkuu amemshukuru Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kutekeleza kwa vitendo mpango wake wa kuvijengea uwezo vyombo
vya ulinzi na usalama nchini.
Mheshimiwa Majaliwa pia amewataka wahitimu hao wakafanye
kazi kwa uzalendo, weledi na kutanguliza kwanza maslahi ya Taifa katika kazi
zao za kila siku. “Kila mmoja akazingatie maadili na miiko ya kazi na akawe
mfano bora wa uadilifu katika kituo atakachopangiwa,” amesisitiza.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa Jeshi la Uhamiaji
wawachukulie hatua kali za kisheria wahitimu ambao watabainika kuwa
wanajihusisha na vitendo viovu ikiwemo rushwa, wizi wa maduhuli ya Serikali,
ama kujiunga na mitandao ya uhalifu wa kiuhamiaji.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kutokana na kuongezeka kwa
teknolojia za kisasa na makosa ya kiuhalifu hususan biashara haramu ya
usafirishaji wa binadamu na uhamiaji haramu, wahitimu hao wanapaswa kuhakikisha
wanapata maarifa mapya mara kwa mara ili waweze kukabiliana na mabadiliko hayo
ya kiteknolojia.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Meneja wa
TARURA mkoa wa Tanga ahakikishe kuwa hadi kufikia mahafali ya mwaka 2024 awe
ameijenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka barabara kuu inayoingia
chuoni hapo.
Kuhusu changamoto ya maji kwa chuo pamoja na wananchi wa
vijiji jirani, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Mamlaka za maji za Mkoa wa Tanga
zihakikishe taasisi hiyo inaunganishwa kwenye mtandao wa maji. “Lakini pia
Katibu Mkuu upo hapa, ona namna ya kuwezesha chuo hiki fedha kwa ajili ya
ujenzi wa tanki la kuhifadhi kama yalivyo mahitaji ya chuo.”
Mapema, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni
alisema awali Jeshi la Uhamiaji halikuwa likitoa mafunzo kwa watumishi wake.
"Mwaka jana ndiyo tulitoa kundi la kwanza la wahitimu,
tunamshukuru Mhe Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa sh. bilioni
1.5 za kuendeleza majengo. Hatukuwa na ajira mpya katika idara ya uhamiaji,
tunamshukuru kwa kuongeza ajira wakiwemo hawa 521 wanaohitimu leo,"
alisema.
Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye ni Mbunge
wa jimbo la Mkinga, Bw. Dunstan Kitandula alisema anashukuru Serikali kwa uwepo
wa chuo hicho na kuongeza: "Tunaiomba Serikali iendelee kuboresha chuo
hiki kwa sababu matamanio yetu ni kuona chuo kinasaidia Afrika Mashariki
yote."
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala aliiomba
Serikali isaidie kuboresha miundombinu ya chuo hicho ikiwemo barabara ya
kuingia chuoni na uwanja wa gwaride. Pia aliomba wajengewe tanki la lita
250,000 ili kutatua shida ya maji chuoni hapo na kwenye vijiji vya jirani.
0 Maoni