Spika wa bunge ataka kufanyika tathimini ya mfumo wa uagizaji wa mafuta

 

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, amesema anafikiri ni wakati muafaka sasa kwa Serikali kufanya tathimini maalum ya kwa ajili ya mfumo mpya wa uagizaji mafuta nchini.

Dkt. Tulia ametoa kauli hiyo leo Bungeni Jijini Dodoma, katika kuonyeshwa kuguswa na kero ya sasa ya mafuta ambayo imekua ikijitokeza katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha adha kwa wananchi.

“Haiwezekani mafuta yanakuwepo wiki mbili, wiki mbili zingine lazima tuanze kutafutana halafu bei zikitangazwa mafuta yanakuwepo,” alisema Dkt. Tulia na kuongeza, “Kama huu mfumo unatupelekea kwenye changamoto nyingi zaidi kuliko ule wa kwanza basi tuangalie namna ya kuuboresha ule wa kwanza”.

Aidha, Spika Dkt. Tulia amesema lakini kama mfumo huu uliopo unatupelekea kwenye mianya ambayo pengine tumeiachia, basi ifanyike tathimini itakayopelekea kubaini pengine hiyo mianya ipo wapi ili tuizibe.

Hivi karibuni, kumekuwapo na uhaba wa mafuta katika baadhi ya maeneo nchini kila inapokaribia kutangazwa kwa bei mpya Jumatano ya kwanza ya mwezi na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), na mafuta kuanza kupatikana pindi tu inapotangazwa bei mpya.

Chapisha Maoni

0 Maoni