Septemba 30 mwisho wa kutumia mfumo wa TANePS- Maswi

 

Taasisi za manunuzi za umma 920, bado hazijapatiwa mafunzo ya kutumia mfumo mpya wa manunuzi wa umma kwa njia ya kidigitali wa NeST, wakati zikiwa zimebakia siku nane tu kabla ya kuachana na mfumo wa zamani wa TANePS, uliokuwa ukisimamiwa na mzabuni kutoka Ugiriki.

Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Bw. Eliakim Maswi wakati akiongea na Wahariri wa habari leo Jijini Dar es Salaam, ambapo amesema ni taasisi za umma 653 tu, ndizo zilizokwishapatiwa mafunzo ya kutumia mfumo mpya.

“Tumeendesha mafunzo kwa taasisi za umma 653 zilizokuwa tayari kupatiwa mafunzo ya mfumo mpya wa NeST, bado taasisi 920, hata hivyo hadi kufikia jana taasisi 400 zimejitokeza kutaka mafunzo na tunatarajia nyingine kuongezeka, “alisema Bw. Maswi.

Aidha, amasema wazabuni 1,508 walipata mafunzo katika vituo mbalimbali vya mafunzo yaliyoratibiwa na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), mafunzo ambayo kwa sasa yanatolewa kwenye kituo kilichopo Iringa katika Chuo Kishiriki cha Mkwawa.

Akiongelea sababu za kuanzisha mfumo mpya wa manunuzi wa umma wa NeST, amesema ni kutokana na mfumo wa zamani wa TANePS ulioanza kutumika Januari mosi 2020 kupitwa na wakati, kutokukidhi mahitaji ya sasa ya PPRA na usimamizi wake kuwa nchi za nje.

“Mfumo wa TANePs ulijengwa na kampuni ya Ugiriki ya European Dynamics na kwa mujibu wa mkataba kampuni hiyo ni mmiliki wa mfumo, lakini pia ni mwendeshaji wa mfumo, huku PPRA na timu yake wakibakia kuwa waangalia tu,” alisema Bw. Maswi na kuongeza “Mkataba wa TANePS unamalizika ifikapo Desemba 31, 2023, mfumo huo unamilikiwa na Ugiriki na unaendeshwa na Ugiriki, mimi nilipofika pale (PPRA) nikasema hii ni nchi yetu lazima tuijenge”.

Amesema mzabuni TANePS alitaka tumlipe dola za Marekani milioni 25 ili Serikali inunue mfumo wake wa kizamani, fedha ambazo sawa na shilingi bilioni 65, wakati nchi kwa kuwatumia wataalamu wake Watanzania kutengeneza mfumo mpya hata shilingi bilioni 10 hazifiki.

Bw. Maswi amesema mfumo wa NeST umetengenezwa na Watanzania na umekidhi matakwa ya PPRA, unaendana na wakati, rahisi kutumika, nyaraka karibu zote zinapatikana kwenye mfumo na umeunganishwa na taasisi zote muhimu za Serikali.

Amesema mfumo wa NeST ambao unatumia lugha ya Kiswahili na Kingereza, ujenzi wake ulianza Julai 18, 2022, na kutokana na jina la TANePS kuwakera watu ilipendekezwa kubadilishwa jina na likapendekezwa jina jipya la National e-Procurement Stystem of Tanzania (NeST).

Serikali imepanga kuzima mfumo wa manunuzi ya umma wa TANePS ifikapo tarehe 30 Septemba 2023, na kuanzisha mfumo mpya wa NeST ambao utaondoa changamoto za awali zikiwemo za rushwa, upendeleo, kukosekana kwa uwazi, matumizi ya muda mrefu na udanganyifu wa wazabuni.

Chapisha Maoni

0 Maoni