WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atapeleka timu maalum ya
uchunguzi wilayani Kigoma ili ifanye uchunguzi wa fedha zinazopotea kinyemela
kupitia mtandao wa watumishi wasio waaminifu.
“Hapa Manispaa mnapokea fedha, zinakaa kwenye akaunti kwa
muda halafu zinapotea, hazijulikani zimefanya nini. Nitaleta timu, waje
wafuatilie hapa Kigoma, waende hadi TAMISEMI ili tuone huo mnyororo unaenda
wapi,” amesema Majaliwa.
Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Ijumaa, Septemba 22, 2023)
wakati akizungumza na viongozi wa dini, Serikali, Chama cha Mapinduzi (CCM) na
watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma na Halmashauri ya Wilaya ya
Kigoma kwenye ukumbi wa NSSF, Kigoma mjini.
Amesema fedha zinazotoka Serikali Kuu huwa zinatumwa na
maelekezo mahsusi ya kwamba zinaenda kufanya shughuli gani; na za makusanyo ya
ndani maamuzi ya matumizi yake ni lazima yafanywe na Baraza lote la Madiwani.
Akitoa mfano, Waziri Mkuu amesema Manispaa ya Kigoma
ilipokea sh. milioni 500 kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI zikakaa kwenye akaunti
kwa muda mrefu lakini baadaye zikatoweka na hazijulikani zilitumika kufanya
nini.
“Kuna kiasi kingine cha shilingi milioni 447 kilitumwa
Kigoma, wakati zinaandaliwa kutoka, Mkurugenzi akazuia. Hongera Mkurugenzi na
uendelee kuzizuia, sisi tunamfuatilia Mkurugenzi aliyekuwepo kwa sababu anajua
zile shilingi milioni 500 zilitokaje,” alisema Majaliwa.
Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Waziri Mkuu
amesema wao wanakabiliwa na matatizo mengi yakiwemo matumizi mabaya ya fedha,
makusanyo kidogo sababu ya malumbano, mawakala kukaa na fedha mikononi badala
ya kuzipeleka benki, Baraza la Madiwani kukosa taarifa za fedha na kutumia
fedha za miradi kulipana posho.
“Kuna watu wamejilipa shilingi milioni 11 zikiwa ni posho ya
safari ya Dodoma. Pia wametumia shilingi milioni sita kufanya service ya gari,
hili ni gari la aina gani? Wengine wametumia shilingi milioni 9 kwenye sherehe
za Siku ya Mtoto wa Afrika na wengine wamejilipa shilingi milioni 14. 8 kwenda
kwenye sherehe za Nane Nane Tabora, hivi mlikaa siku ngapi huko?”, alihoji
Waziri Mkuu.
Amesema kuna tume ya TAMISEMI ilikwenda kufanya uchunguzi
kwenye Halmashauri hiyo kuhusiana na matatizo hayo. Hivyo, ameitaka tume hiyo
ikamilishe kazi yake haraka na kuiwasilisha kwa Waziri wa Nchi, OR TAMISEMI.
“Tume ikamilishe kazi haraka, akabidhiwe Waziri. Namwagiza Mheshimiwa Waziri
Mchengerwa akipokea taarifa ya tume hiyo, aje Kigoma achukue hatua,” amesema.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaasa watumishi wa
Halmashauri zote mbili waache makundi kwani yanasababisha migongano na
kuzorotesha utoaji huduma kwa wananchi. “Migogoro yenu inasababisha upotevu wa
rasilimali watu na fedha.”
Waziri Mkuu amemaliza ziara yake ya siku tatu mkoani Kigoma
na ameanza ziara ya siku tatu mkoani Kagera.
0 Maoni