Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) itaanzisha huduma ya
upandikizaji Ini ifikapo mwaka 2025 ikiwa ni mwendelezo wa azma ya Serikali
kuhakikisha kwamba huduma za ubingwa bobezi zinapatikana nchini.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed
Janabi wakati akifungua mafunzo ya awali ya uchunguzi na matibabu ya
magonjwa ya ini yaliyofanyika hospitalini katika kuelekea kwenye kongamano la
wataalamu wa magonjwa Ini Barani Afrika (COLDA) linalotarajiwa kufanyika
September 7 hadi 9 Jijini Dar es Salaam.
Prof. Janabi amesema katika kuelekea hatua ya upandikizaji
Ini mafunzo mbalimbali ya wataalamu yanaendelea kutolewa kupitia Kituo cha
kutoa mafunzo, uchunguzi na matibabu ya kibobezi ya Magonjwa ya Mfumo wa
Chakula na Ini katika Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika kilichopo
MNH kilichoanzishwa mwaka 2012 kwa ushirikiano na ufadhili wa Taasisi ya Munich
Foundation ya Ujerumani, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili
hivyo kuifanya hospitali kuwa miongoni mwa vituo vichache vyenye hadhi ya namna
hii Barani Afrika, vituo vingine vipo Rabat Morocco, Johannesburg Afrika ya
Kusini na Cairo Misri.
Amesema kuwa kongamano la wataalamu wa magonjwa Ini Barani
Afrika linalotarajiwa kufanyika Septemba 7 hadi 9 ni moja ya maandalizi ya
kusaidia huduma za upandikizaji Ini kuanza kufanyika nchini kwa kuwa litatoa
fursa ya wataalamu kujifunza, kujadili na kupanga mwendelezo wa mafunzo ya mara
kwa mara ya ndani na nje ya nchi ambayo yatawajengea uwezo wataalamu wetu
kuanzisha huduma ya upandikizaji Ini nchini
“Hii safari ni ndefu na nzito lakini tunaamini kwa msaada wa
Serikali na wadau mbalimbali, tutafanikiwa kwani hadi sasa kituo kina uwezo wa
kutoa huduma kwa wagonjwa waliofanyiwa huduma hiyo nje ya nchi wanaporejea hapa
nyumbani tofauti na awali ambapo walilazimika kurudi nje ya nchi. Jambo hili
linaenda sambamba na uboreshaji wa maabara za kiuchunguzi wa patholojia,
uchunguzi wa damu, uchunguzi wa radiolojia na tiba radiolojia na uboreshaji wa
vyumba vya wagonjwa mahututi” amesisitiza Prof. Janabi.
@wizara_afyatz @ikulu_habari @ikulu_mawasiliano
0 Maoni