Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene (Mb) ametaka Madaktari na Walimu wasiwe wasimamizi wa
miradi ya ujenzi inayotekelezwa katika maeneo yao ya kazi huku akisisitiza kuwa
sio taaluma yao na ni matumizi mabaya ya rasilimaliwatu.
Badala yake, ameutaka Uongozi wa Halmashauri zote nchini hususan
Halmashauri ya Mpwapwa kuhakikisha inaachana utaratibu huo, iajiri Wataalam wa
fani ya ujenzi kwa ajili ya kusimamia miradi yote itakayokuwa ikitekelezwa
katika Halmashauri hiyo ili iwe ya viwango vya ubora kama ambavyo baadhi ya Halmashauri
zingine zinafanya.
Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akikagua ujenzi wa
mradi wa vyumba viwili vya maabara wenye thamani ya Shilingi milioni 60 unaoendelea
katika Shule ya Sekondari Rudi iliyopo katika Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya
wilaya ya Mpwapwa, Mkoani Dodoma, ikiwa ni ziara ya kukagua utekelezaji wa
miradi ya ujenzi katika Jimbo hilo.
" Kwa sasa majengo yetu yanajengwa na Walimu na
Madaktari na badala ya kujengwa na Wahandisi wa ujenzi, hili halikubariki hata
kidogo, amesititiza Mhe.Simbachawene.
Ameweka angalizo kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa
imekuwa haifanyi vizuri katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi
kutokana na usimamizi hafifu kwa sababu Wasimamizi wanaopewa jukumu hilo sio
taaluma yao.
Amefafanua kuwa Walimu au Madaktari wanaosimamia miradi hiyo
ujenzi sio kwamba ni wabadhirifu lakini kwa kuwa sio taaluma yao hivyo ni
vigumu kuona na hata kushauri pale ujenzi unavyojengwa chini ya kiwango.
Amesema limekuwa ni jambo la kawaida kama mradi afya
unatekelezwa basi msimamizi wa ujenzi atakuwa Daktari, vivyo hivyo kama ujenzi
wa madarasa basi msimamizi atakuwa Mwalimu.
" Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ajirini wataalamu wa
ujenzi hata kwa ajira ya mkataba ili waweze kusimamia ujenzi haiwezekani Miradi
yetu isimamiwe na Walimu na Madaktari kwani wao sio Wahandisi wa majengo,”
alisema Mhe. Simbachawene.
Ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan moja ya msisitizo wake katika itekelezaji wa
miradi ni lazima iendane na thamani ya fedha.
Katika hatua nyingine, Mhe.Simbachawene amewasihi madiwani
ya Halmashauri ya Mpwapwa kujiepusha na tabia ya kuchukua tenda ya miradi ya
ujenzi inayotekelezwa ndani ya Halmashauri hiyo ili kuepusha mgongano wa
maslahi baina yao.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,
Mhe.Richard Maponda amesema atahakikisha wanasimamia maelekezo hayo ili kodi za
watanzania zinazotumika katika kutekeleza miradi hiyo iendane na thamani halisi
ya fedha.
0 Maoni