WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtaka Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba ahakikishe anaweka utaratibu mzuri wa
uendeshaji wa soko la kimataifa la mazao ya uvuvi la Magarini ikiwemo kuajiri
mtumishi wa Serikali atakayesimamia makusanyo.
“Lete Afisa Mapato hapa badala ya kutoa ajira kwa vibarua;
eneo hili litawasaidia kupata mapato mengi ambayo yatasaidia kuendesha soko
hili ikiwemo kuweka taa za barabarani. Wavuvi wenu wahudumiwe na wasaidiwe ili
waweze kufanya kazi zao kwa urahisi,” amesema wakati akitoa maelekezo kwa
Mkurugenzi huyo, Dkt. Peter Nyanja.
Ametoa wito huo jana wakati akizungumza na wananchi wa
Magarini na wafanyabiashara mara baada ya kukagua bandari ya Magarini na Soko
la Kimataifa la mazao ya Uvuvi la Katembe - Magarini lililopo kata ya
Nyakabango, wilayani Muleba, mkoani Kagera.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali imeweka utaratibu
kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuwawezesha wavuvi kufanya shughuli zao
kwa tija. “Rais Dkt. Samia ameweka nguvu ili kuwanufaisha wavuvi ikiwemo
kununua boti 1,200 kwa ajili ya vikundi vya wavuvi ili kuwawezesha wavue mbali
zaidi.”
Katika mwaka fedha 2022/2023, soko hilo linalohudumiwa na
Mamlaka ya Bandari Tanzania, Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Halmashauri ya
Muleba lilizalisha tani milioni 26.96 za dagaa na samaki kutoka visiwa vya
Bumbire, Maziga, Ikuza, Kerebe na Goziba.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuelekeza Meneja
Bandari - Kanda ya Ziwa Victoria, Bw. Erasto Lugege afanye maboresho ya bandari
ya Magarini kwenye eneo la jengo la abiria na gati.
Vilevile, amezitaka taasisi za Mamlaka ya Bandari Tanzania
(TPA), Mamlaka ya HIfadhi za Taifa (TANAPA) na Halmashauri ya Wilaya zikae
pamoja na kupanga vizuri eneo hilo ili liwe kivutio.
“Malengo yetu ni kuongeza kituo cha TANAPA ili shughuli za
utalii zianzie hapa kwenda kwenye hifadhi ya Rubondo badala ya kuzunguka hadi
Chato,” alisema Majaliwa.
Akitoa taarifa yake, Meneja Bandari - Kanda ya Ziwa
Victoria, Bw. Erasto Lugege alisema kwenye bajeti ya 2023/2024 wanatarajia
kuboresha gati hilo ambalo lilifunikwa na maji tangu mwaka 2020 kutokana na
mvua kubwa zilizonyesha kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
0 Maoni