NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko
ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuhakikisha
inapitia mfumo mzima wa upangaji wa bei ya mafuta ili kuwezesha bei
zinazopangwa zilingane na uhalisia wa maisha.
Dkt. Biteko ametoa kauli hiyo Jjini Dar es Salaam akizungumza na
Wafanyakazi wa EWURA ambapo amewasihi Wafanyabiashara wa mafuta ya dizeli na
Petroli nchini kuwa waaminifu wakati wakiendelea kutoa huduma kwa Watanzania.
Dkt. Biteko amekumbushia kuwa, pamoja na kuwa ni
Wafanyabishara lakini pia wanatoa huduma kwa Wananchi.
‘’Naomba Wafanyabiashara wenye leseni za biashara ya mafuta
nchini watambue kuwa wana wajibu wa kuhudumia watanzania ili wapate bidhaa
hiyo, tunajua kuwa kiwango cha uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi kimepungua
lakini Serikali inaendelea kulifanyia kazi,” amesema Dkt. Biteko.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Biteko amesema,
Serikali inafanya kazi kubwa ili kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa
mafuta nchini inamalizika.
“Wazalishaji wa mafuta duniani wamepunguza uzalishaji lakini
mahitaji ya mafuta yameongezeka kwa sababu ya shughuli za kiuchumi
zinazotekelezwa ikiwemo ununuzi wa magari na ujenzi wa viwanda vya kuzalisha
malighafi mbalimbali,” amesema Dkt. Biteko.
Aidha, amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo Serikali
imeanza kuwekeza katika ujenzi wa vituo vya Gesi Asilia - CNG ili kuhamasisha
wananchi kuanza kutumia magari yanayotumia mfumo wa Gesi Asilia ikiwemo magari
ya Serikali.
Amefafanua kuwa faida zitakazopatika kama magari yaliyokuwa
yakitumia mafuta yakianza kutumia mfumo wa uendeshaji unaotumia Gesi Asilia -
CNG, gharama za uendeshaji wa magari hayo zitapungua na mafuta yaliyokuwa
yakitumiwa na magari hayo yatatumika kuendesha mitambo iliyopo viwandani.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati,
Mhandisi Felchesmi Mramba na watendaji wengine kutoka wizara ya Nishati na
EWURA.

0 Maoni