Barabara ya Mtwara- Mnivata yenye urefu wa km 50, ni sehemu
ya barabara ya kusini itokayo Mtwara- Newala hadi Masasi kupitia Wilaya za
Tandahimba na Newala yenye urefu wa km 210.
Barabara hiyo inatajwa kupitia maeneo ya kimkakati katika
mtandao wa barabara ambako korosho hulimwa kwa wingi katika Wilaya za
Tandahimba na Newala, hivyo itaunganisha wakulima na masoko kupitia Bandari ya
Mtwara na Kiwanja cha Ndege cha Mtwara kwenda katika maeneo mengine ya ndani na
nje ya nchi.
Akizungumza leo mkoani Mtwara wakati wa uzinduzi wa barabara
hiyo, Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema “Mara ya mwisho
nilipopita kwenye kampeni wananchi mliomba kupata barabara, sasa tayari
kilomita 50 zimeshakamilika na zilizobaki lazima tuzikamilishe hadi Masasi kwani
barabara hii ni muhimu sana hasa kwa kusafirisha mazao kutoka mashambani kwenda
sokoni”.
Aidha, Rais Samia amewataka wananchi mkoani humo kudumisha
amani, kufanyakazi kwa bidii na kuzalisha mazao kwa wingi ili Serikali ipate
fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ya kwa faida ya Watanzania.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS),
Mhandisi Mohamed Besta amesema kuwa utekelezaji wa mkataba kwa sehemu ya Mtwara-Mnivata
(km 50) umegharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
asilimia 100.
“Hadi kukamilika kwa mradi huu, jumla ya shilingi
78,401,225,420.37 zimelipwa kwa Mkandarasi, shilingi 4,614,877,406.77 zimelipwa
kwa Mhandisi Mshauri na Shilingi 70,435,260.94 zimelipa fidia ya mali na ardhi
kwa wananchi walioathiriwa na Mradi kwa Mujibu wa sheria”, ameeleza Mhandisi
Besta.
Akifafanua zaidi, Mhandisi Besta amesema upembuzi yakinifu
na usanifu wa kina na uandaaji wa nyaraka za zabuni wa Barabara ya Mtwara -
Newala - Masasi (km 210) ikijumuisha Daraja la Mwiti ulifanywa na Kampuni ya
Mult-Tech (Pty) Ltd ya kutoka nchini Botswana kwa ushirikiano na Kampuni ya
Unitec Civil Consultants Ltd ya Tanzania, kwa gharama ya shilingi
1,280,831,600.00 bila kodi ya ongezeko la thamani na kazi hiyo ilikamilika
mwezi Desemba, 2015.
Aidha, kulingana na usanifu, sehemu isiyo na makazi, barabara
hiyo imejengwa kwa upana wa mita 9.5 ambapo mita 6.5 ni njia ya magari na mita
1.5 kila upande ni mabega ya barabara kwa ajili ya watembea kwa miguu. Sehemu
za makazi barabara imejengwa kwa upana wa jumla wa mita 10.5 ambapo mita 6.5 ni
njia za magari na mita 2.0 kila upande ni mabega ya barabara kwa ajili ya
watembea kwa miguu.
Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
0 Maoni