Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Wakala wa Barabara
Vijijini na Mijini (TARURA) kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha wahandisi
wazawa wanashiriki kwenye ujenzi wa miradi mbalimbali nchini.
Amesema kuwa kupitia utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo
wa Miaka Mitano wa Tanzania, unaolenga kupunguza ukosefu wa ajira kutoka 9%
hadi 8% ifikapo 2025/26, Serikali inatarajia kutimiza azma yake ya kuhakikisha
inazingatia ushiriki wa Watanzania kwenye sekta ya ujenzi ili kukuza ujuzi.
Majaliwa ameyasema hayo jana alipomuwakilisha Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwenye maadhimisho ya siku wahandisi, katika ukumbi wa
Mlimani city, Dar es Salaam.
“Wizara ya Ujenzi pamoja na bodi ya wahandisi inalifanyia
kazi suala la ushiriki mdogo wa wazawa katika miradi ya maendeleo, hii ni
changamoto ambayo mmeiibua, Serikali sasa imeliweka kwenye mpango wa
kuhakikisha changamoto inafanyiwa kazi ili kuongeza idadi ya wazawa kushiriki
katika kazi za ndani,” alisema Majaliwa.
Amesema kuwa Serikali imedhamiria kuhakikisha wahandisi
wazawa wananufaika kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali “miradi hii ni
fursa kwenu, natoa rai mjipange na kufanya juhudi za makusudi kila mmoja kwenye
eneo lake ahakikishe kwa uzalendo alionao na mapenzi kwa nchi yake kuwa kinara
katika sekta unayosimamia ili kulijenga taifa letu”.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameielekeza Bodi ya Usajili wa
Wahandisi iandae mpango mahsusi wa kuwaendeleza wahandisi wanawake ili waweze
kusajiliwa kwa wingi zaidi wanapohitimu masomo “Suala hili litekelezwe kwa
ushirikiano na wadau wengine wa uhandisi”
Naye Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenye
amesema kuwa Serikali inatambua mchango wa taaluma ya uhandisi katika sekta
mbalimbali za kiuchumi kupitia uanzishaji wa viwanda, uendelezaji wa
miundombinu ya kilimo, nishati, maji, uvuvi, utumiaji mzuri wa rasilimali na
malighafi, usafiri na mawasiliano.
“Katika mwaka 2023/2024 Serikali imetenga miradi maalum ya
ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kwa ajili ya wakandarasi wanawake,
ambao zabuni zitashindanishwa kwa makandarasi wanawake tu,” alisema Mhandisi
Kasekenye.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi Mhandisi
Menye David Manga Amesema kuwa bodi inatarajia kufanya mageuzi makubwa ya
teknolojia ili kuhakikisha wahandisi waliosajiliwa na wenye sifa wanakuwepo wa
kutosha kwa ajili miradi mbalimbali nchini ili kujenga dhana halisi ya
ushirikishwaji wa wazawa ‘local content’ “Tutakuwa na mageuzi katika sheria na
kanuni zetu ili kuongeza usajili wa wahandisi”.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni