Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amewataka Wachimbaji wa
Makaa ya mawe na wadau wenye wateja wa makaa hayo kutoka nje ya nchi kuitumia
Bandari ya Mkoani Mtwara ili kusafirisha bidhaa katika bandari hiyo.
Dkt. Biteko ametoa wito huo jana alipotembelea na kuzungumza
na uongozi wa bandari ya Mtwara ili kujionea shughuli zinazofanywa hususan
katika usafirishaji wa makaa ya mawe kwenda nje ya nchi.
Amesema kuwa, miundombinu katika bandari ya Mtwara
inaendelea kuboreshwa ili kuhakikisha makaa ya mawe yanafika kwa wakati nje ya
nchi yalipo masoko ya uhakika ya bidhaa hiyo.
"Nawapongeza sana kwa kutengeneza mazingira mazuri
angalau wanajitahidi sana kuhakikisha makaa ya mawe yanayofika hapa yanajazwa
kwenye meli na kusafirisha nje ya nchi," amesema Biteko.
Dkt. Biteko ameongeza kuwa, biashara ya makaa ya mawe
imekuwa kubwa hivi karibuni kutokana na uhitaji wa makaa hayo duniani na hivyo
bandari ya Mtwara kufanya shughuli nyingi za usafirishaji wa makaa nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa, Mamlaka ya
Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekuwa msaada mkubwa katika usafirishaji
wa bidhaa zinazotokana na Sekta ya Madini kwenda kwenye masoko ya nje kwa
urahisi zaidi.
Pia, ameipongeza Kampuni ya Ruvuma Coal inayochimba makaa ya
mawe kwa kuagiza mtambo ambao utakua mkanda wa kusafirisha makaa moja kwa moja
hadi kwenye meli kwa kushirikiana na Mamlaka ya bandari.
"Mitambo hii itatusaidia sana kupunguza muda wa kujaza
wa mizigo kwenye meli utakua mfupi zaidi kuliko hivi sasa," amesema Dkt.
Biteko.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mtwara Mhandisi
Ephraim Mushi amesema, bandari ya Mtwara imepokea meli zinazofika kupakia makaa
ya mawe kwenda nje ya nchi hususan nchi ya India, Senegal, France, Egypt,
Poland, Ghana, Kenya, Congo na China.
Aidha, Ofisi ya Afisa Madini Mtwara imekuwa na jukumu la
utoaji wa vibali (Export Permit) na kusimamia upakiaji wa makaa ya mawe kwa
kushirikiana na taasisi zingine.
Madini mengine yanayopatikana mkoani Mtwara ni kama vile
madini ya ujenzi, dhahabu, shaba, chokaa, udongo mwekundu, chuma, chumvi,
Kinywe na Madini Mazito ya Mchanga (Heavy Mineral Sand).
0 Maoni